Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumechoshwa na mzunguko wa vita tunachotaka ni amani: Wanawake wa Tambura Sudan Kusini

Familia za waliokimbia makaiz yao sababu ya machafuko wakiwa wamepata hifadhi huko Tambura nchini Sudan Kusini
UNMISS
Familia za waliokimbia makaiz yao sababu ya machafuko wakiwa wamepata hifadhi huko Tambura nchini Sudan Kusini

Tumechoshwa na mzunguko wa vita tunachotaka ni amani: Wanawake wa Tambura Sudan Kusini

Amani na Usalama

Maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao huko Tambura, jimbo la Equatoria Magharibi, tangu ghasia zilipozuka upya mwaka 2021 nchini Sudan Kusini. Hadi leo, wengi wao bado wanaishi kambini bila chakula cha uhakika, huduma za afya wala usalama huku wanawake na watoto wakibeba mzigo mkubwa zaidi wa mateso hayo. 

Kupitia video ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo UNIMSS   baadhi ya wanawake waathirika wanaosihi katika kambi ya wakimbizi wa ndani wanaeleza madhila yao na kutaka vita ikome.

Tambura, katika jimbo la Western Equatoria, familia nyingi bado zinaishi na makovu ya mzozo uliozuka mwaka 2021. Maelfu walilazimika kufunga virago na kuyakimbia makazi yao, na hadi leo, miaka kadhaa baadaye, wengi bado wamekwama kwenye kambi za wakimbizi wa ndani wakiishi kwa hofu, udhaifu na bila uhakika wa mustakbali wao.

Miongoni mwao ni Geonina Louis Wanja, mjane anayelea watoto wake peke yake. Anaeleza kuwa maisha kambini ni mapambano ya kila siku ya kuendelea kuishi. “Mgogoro ulipoanza, hatukufurahi kama wanawake, watoto wetu nao hawana furaha. Hata hapa kambini hatuko salama. Mimi mume wangu amefariki dunia, nipo hapa na watoto wangu ambao ni yatima. Ni nani atanisaidia na hawa watoto?”

Kama wakimbizi  wengine wengi, Geonina anaishi katika hofu ya kudumu sio tu ya njaa au maradhi, bali pia ya kile kitakachotokea ikiwa ghasia zitarejea. Catherine Pijani, naye akiwa kambini na binti zake, anashiriki hofu hiyo.

“Nipo hapa na mabinti zangu wanne. Unaona hali yetu. Hofu yetu kubwa ni kutokuwa salama, huenda wakaja kutubomolea hapa kwenye hema. Tunaishi hapa na likitokea jambo lolote, hakuna atakayeshuhudia. Tunaishi kwa neema ya Mungu pekee.”

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini wanaendelea kufanya doria kambini, wakidumisha hali ya usalama kiasi. Lakini kwa wanawake wengi, amani ya kweli ina maana kubwa zaidi. Gloria Marko Juma anaamini mazungumzo ndio njia pekee ya kutoka kwenye mzunguko huu wa vita na kutoka hapa.
“Wanaume ndio wanasababisha huu mgogoro. Kama tungebaki wanawake pekee, mgogoro huu ungekua umekwisha. Kinachopaswa kufanyika ni kuwaleta pamoja pale Freedom Square, Wazande na Wabalanda wakae kwenye mazungumzo. Tumechoka, wanapaswa kuzungumza ili turudi nyumbani.”

Kwa wanawake wa Tambura, amani sio ndoto ya mbali. Ni nafasi ya kurudi nyumbani, kuishi bila hofu, na kujenga upya maisha ya watoto wao. Hadi hapo, wanasubiri wakiwa kwenye mahema, wakishikilia ndoto ya  tumaini.