Watoto wanne wameuawa katika mashambulizi ya Urusi usiku kucha ya Urusi dhidi huko Kyiv
Watoto wanne wameuawa katika mashambulizi ya Urusi usiku kucha ya Urusi dhidi huko Kyiv
Mashambulizi ya Urusi usiku kucha kuamkia leo dhidi ya miji ya Ukraine, yakiwemo katika mji mkuu Kyiv, yamesababisha vifo vya watoto wanne na kujeruhi makumi ya watu, yameripoti leo mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, mwathiriwa mdogo zaidi alikuwa na umri wa miaka miwili na nusu.
Shirika hilo limetoa video ikionesha moshi mkubwa ukifuka katika jengo la makazi mjini Kyiv, lenye shimo kubwa sehemu ya paa lake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres naye alilaani mashambulizi hayo akisisitiza kuwa kulenga raia na miundombinu ya kiraia kunakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, jambo lisilokubalika na lazima likome mara moja. Ameendelea kusisitiza haja ya usitishaji mapigano utakaosababisha amani ya haki, ya kina na endelevu nchini Ukraine.
Hakuna palipo salama Ukraine
Akizungumza na UN News baada ya kutembelea jengo lililoharibiwa na kukutana na wakazi wake, Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine, Munir Mammadzade, amesema hakuna sehemu salama nchini humo kwa sasa.
Alibainisha kuwa tahadhari ya mashambulizi ya anga Kyiv ilidumu kwa takribani saa 12.
Afisa huyo wa ngazi ya juu amelaani mashambulizi yanayoendelea ya makombora na droni, akieleza kuwa juhudi za uokoaji bado zinaendelea na idadi ya vifo na majeruhi huenda ikaongezeka.
Duru za habari pia zimetaja uharibifu zaidi wa miundombinu ya kiraia, ikiwemo reli na miundombinu ya nishati, hasa ikizingatiwa majira ya baridi yanakaribia.
Changamoto ya majira ya baridi
Mammadzade ameonya kuwa kushuka kwa joto au msimu wa baridi ndilo tishio kubwa zaidi kwa familia zilizo Kyiv na maeneo ya mstari wa mbele wa vita. Ameomba msaada wa wahisani kusaidia mpango wa UNICEF wa kukabiliana na baridi, unaokabiliwa na upungufu wa ufadhili kwa asilimia 40.
Watoto na shule
Wakati huo huo, watoto nchini Ukraine wanajiandaa kurejea shuleni huku wakikabili hofu ya mashambulizi ya anga yanayokuwa jambo la kawaida.
Hata hivyo, athari za kisaikolojia kwa watoto ni kubwa, amesema ikiwemo msongo wa mawazo na kukata tamaa.
“Watoto wengi wanasema hawana ndoto wala matumaini. Wanachohitaji ni amani ili warejee kwenye maisha ya kawaida,” amesema Mammadzade, akionya kuwa athari za vita zitaendelea kwa vizazi vijavyo hata kama vita vingeisha leo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena kwamba usitishaji mapigano wowote lazima uheshimu kwa ukamilifu uhuru, mamlaka na mipaka ya Ukraine kama inavyotambuliwa kimataifa, kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio husika.