Watu wa Haiti wako katika 'kimbunga' kamili cha mateso - Guterres
Watu wa Haiti wako katika 'kimbunga' kamili cha mateso - Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema watu wa Haiti wanapitia dhoruba kamili ya mateso.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema watu wa Haiti wanapitia dhoruba kamili ya mateso.
Amesema hayo yanaendelea huku mamlaka za serikali zikisambaratika wakati ghasia za magenge zikizidi kushamiri kwenye mji mkuu Port-au-Prince na kuenea zaidi, jambo linalolemaza maisha ya kila siku na kulazimisha familia kukimbia makazi yao.
Guterres amehutubia Baraza hilo katika kikao maalum kuhusu hali ya kibinadamu na ulinzi wa watoto nchini Haiti kilichoitishwa na Panama ambayo ndiyo inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Agosti.
“Raia wako katika hali ya kuzingirwa huku kukiwa na ripoti za kusikitisha za ubakaji na ukatili wa kingono. Hospitali na shule zimekuwa zikishambuliwa mara kwa mara, na utawala wa sheria umesambaratika kabisa.,” amesema Katibu Mkuu.
Akifafanua kwa kina Guterres amesema “athari za kibinadamu ni kubwa mno, watu milioni 1.3 – nusu yao wakiwa watoto – wamekimbia makazi yao, na watu milioni 6 wanahitaji msaada wa kibinadamu.”
Ameongeza kuwa “Haiti sasa imo miongoni mwa maeneo matano duniani yenye njaa kali ya kutisha . Wahudumu wa misaada – hasa wale wa ndani – wamekuwa wakilengwa na vitisho vya ghasia, uporaji na utekaji nyara.”
Wahudumu wa kibinadamu wamesalia Haiti licha ya changamoto
Bwana Guterres amesisitiza kuwa pande zote lazima ziheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kwamba wafanyakazi wa misaada, pamoja na vifaa na vituo vyao, ni lazima vilindwe.
Licha ya hatari zilizopo, amesema wahudumu wa misaada bado wako nchini Haiti wakitoa chakula, maji, dawa, na hifadhi. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu pekee, waliweza kuwafikia watu milioni 1.3.
Ufadhili hautoshi
Hata hivyo, amesema Haiti bado inapuuzwa kwa kiasi kikubwa na haipati ufadhili wa kutosha. Kwa mwaka 2025, Umoja wa Mataifa unahitaji dola milioni 908 kusaidia watu milioni 3.9, lakini ni chini ya asilimia 10 tu ya fedha hizo ndizo zilizopatikana, na hivyo kuifanya Haiti kuwa ombi la kibinadamu lililopata ufadhili mdogo zaidi duniani.
Kwa sababu hiyo, Guterres ameonya kuwa zaidi ya watu milioni 1.7 wako hatarini kutopokea msaada wowote, akisisitiza kuwa hili si pengo la kifedha bali ni dharura ya maisha au kifo, na akatoa wito kwa wafadhili kuchukua hatua kabla ya shughuli za kuokoa maisha hazijasimama kabisa.
Katibu Mkuu alieleza kuwa watoto ndio wanaobeba mzigo mzito zaidi wa janga hili. Katika ripoti yake ya mwaka kuhusu watoto na migogoro ya kivita, Haiti iliorodheshwa miongoni mwa nchi 5 za juu zaidi kwa ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto mnamo mwaka 2024.
“Watoto wanatekwa nyara na kuuawa, wanatumikishwa na makundi ya waasi, na wanakumbwa na ukatili wa kutisha wa kingono – ikiwemo ubakaji wa magenge. Uhalifu huu unachafulia miili, akili, na mustakabali wa watoto hawa.” Amesema Guterres, akieleza kuwa Umoja wa Mataifa umethibitisha ukiukwaji mkubwa 2,269 dhidi ya watoto 1,373 mwaka jana – ongezeko karibu mara tano ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Amesema hii inajumuisha watoto 213 waliouawa, 138 waliopata ulemavu, na watoto 302 waliotumika na kuajiriwa na makundi yenye silaha.
Aidha, ameeleza kuwa walithibitisha matukio 566 ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto – yakiwemo matukio 160 ya ubakaji wa magenge, jambo linaloonesha wazi jinsi uhalifu huu unavyotumika kama silaha ya hofu na udhibiti.
Huduma za msingi zimeporomoka
Amesema huduma za msingi zimeporomoka. Uhamaji mkubwa wa watu umeacha watoto bila elimu, huduma za afya, au usalama. Kufikia Aprili, alibainisha kuwa ghasia za magenge zilikuwa zimekatiza masomo ya wanafunzi 243,000.
Kuhusu Mkataba wa Kukabidhi wa mwaka 2024 unaosimamia mikakati yote ya mpito, ikiwemo kuanzishwa kwa serikali ya mpito na kukabidhi watoto wanaotumikishwa, Guterres amesema ni hatua muhimu katika kulinda watoto waliowekwa kizuizini kwa tuhuma za kuhusika na makundi yenye silaha.
Hata hivyo, ameonya kuwa utekelezaji wake bado ni wa kusuasua.
Mathalani mazingira katika kitu o cha kujumuisha watoto waliotumikishwa bado ni ya kusikitisha.
Amewahimiza viongozi wote kutekeleza mkataba huo wa kufanikisha Mpito
Ametamatisha kwa kusisitiza kuwa “wahalifu wote lazima wawajibishwe,” na akatoa wito kwa Baraza hilo kupatia kipaumbele ulinzi wa watoto.