Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Wapalestina wanashuhudia hofu zao mbaya zaidi zikitimia mbele ya macho yao

Mwonekano wa kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina. Mwakilishi Mkazi na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa UN, Ramiz Alakbarov (kwenye skrini), anatoa taarifa kwa wajumbe.
UN Photo/Loey Felipe
Mwonekano wa kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina. Mwakilishi Mkazi na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa UN, Ramiz Alakbarov (kwenye skrini), anatoa taarifa kwa wajumbe.

Gaza: Wapalestina wanashuhudia hofu zao mbaya zaidi zikitimia mbele ya macho yao

Amani na Usalama

“Kwa njia isiyoelezeka, watu wa Gaza sasa wanakabiliwa na ongezeko lingine hatari la mapigano,” amesema Naibu Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati mbele ya Baraza la Usalama leo Jumatano, akirejelea tangazo la Israel la kutwaa Jiji la Gaza.

Katika kikao cha chombo hicho cha kufanya maamuzi kuhusu hali ya Ukanda wa Gaza, Ramiz Alakbarov amerejelea tangazo la Agosti 8 kuhusu jeshi kutwaa mji mkuu wa eneo hilo la Palestina, akibainisha kuwa operesheni hiyo inaendelea.
 
“Kwa watu waliokuwa tayari wanahangaika kuishi, Wapalestina wa Gaza sasa wanashuhudia hofu zao mbaya zaidi zikitimia mbele ya macho yao,” amesema.
 
Akitaja kuwa zaidi ya asilimia 86 ya Ukanda tayari upo ndani ya maeneo ya kijeshi ya Israel, ameonya kuwa upanuzi wa operesheni za kijeshi katika Jiji la Gaza “utakuwa na madhara ya kutisha,” ikiwemo kuhamishwa kwa mamia ya maelfu ya watu.
 
Alakbarov amelaani mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,550 tangu Julai 23 pekee, na kusisitiza kwamba waandishi wa habari wamekuwa miongoni mwa walengwa. Tangu Oktoba 7, 2023, idadi ya waandishi wa habari waliorekodiwa na Umoja wa Mataifa imezidi 240.
 
Ameongeza kuwa vyanzo vya Israel vinakadiria kuwa mateka 50 bado wako Gaza, ambapo 28 kati yao wanaaminika wamefariki.
 
Mjumbe huyo ameonya kuwa haya yote yanatokea katika muktadha tete wa kikanda, ambapo vurugu na mvutano vinaendelea kuutikisa Mashariki ya Kati: “Wiki hii pekee, kulikuwa na mashambulizi ya kurushiana makombora kati ya Wahouthi nchini Yemen na Israel, mashambulizi ya Israel yanayoendelea nchini Lebanon, na uvamizi wa vikosi vya Israel nchini Syria.”
 
“Hali hii ya kutisha inalazimisha kuchukua hatua thabiti kubadili hali ya sasa, kuanzia na usitishaji wa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote. Kinachohitajika ni hatua za dhati za kusuluhisha mzozo, kukomesha ukaliaji wa mabavu, na kurejesha mwelekeo wa kisiasa,” amesema, akisisitiza kuwa suluhu ya mataifa mawili bado ndiyo njia pekee ya haki na ya kudumu kwa mzozo wa Israel na Palestina.
Hata hivyo, eneo linalotarajiwa kwa ajili ya taifa la baadaye la Palestina linaendelea kupungua, na uhalisia wa ukaliaji haramu na ghasia zisizoisha unakua kwa kasi, amelalamika.
 
Kwa hiyo, Alakbarov amehitimisha kwa kutoa wito wa mshikamano wa kimataifa ili kuchukua hatua kwa manufaa ya njia ya amani: “Kwa Gaza iliyoingia katika hali mbaya inayokinzana na utu wa msingi, na kwa Ukingo wa Magharibi unaokabiliwa na vitisho halisi kwa uwepo wake wa muda mrefu, hatuwezi kusubiri tena.”
 

Njaa Gaza ni janga lililosababishwa makusudi

 
Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, kwa upande wake, amesisitiza kuwa njaa Gaza, iliyothibitishwa Agosti 22, ni matokeo ya miezi 22 ya kuwekewa vizuizi na kunyimwa upatikanaji wa vifaa vya kimsingi pamoja na kudorora kwa mifumo ya afya na lishe.
Joyce Msuya ameeleza kuwa watu milioni 2.1 wanateseka kwa njaa Gaza, na akafafanua kuwa njaa inazidi kusambaa katika mkoa huo na inatarajiwa kufika Deir el-Balah na Khan Yunis kufikia mwishoni mwa Septemba.
 
Joyce Msuya (kwenye skrini), Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, akitoa taarifa kwa kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina.
UN Photo/Loey Felipe
“Tuwe wazi: njaa hii si matokeo ya ukame au aina yoyote ya janga la asili,” amesisitiza, akibainisha kuwa ni janga lililosababishwa katikati ya mzozo uliosababisha vifo, majeraha, uharibifu, na uhamishaji mkubwa wa raia kwa lazima.
 
Njaa Gaza pia ni matokeo ya kuangamizwa kwa mfumo wa uzalishaji chakula, ambapo asilimia 98 ya ardhi inayolimika imeharibiwa au haifikiwi, na mifugo imeangamizwa, amefafanua Naibu Mratibu wa misaada ya dharura.
 
Ingawa amekiri kuongezeka kwa misaada inayoingia Gaza wiki za karibuni, Msuya amerudia kusisitiza uharaka wa kuhakikisha kwamba vifaa muhimu vinaingia kwa wingi na kwa utaratibu wa kudumu, kwa kuwa msaada unaoingia sasa “hautabadili au kusimamisha njaa.”
 
“Tunahitaji mengi zaidi,” amesisitiza, akihimiza Baraza la Usalama kuchukua hatua za haraka.