Ulinzi wa watoto unahitajika bila kutetereka wakati huu mizozo ikishamiri – UN
Ulinzi wa watoto unahitajika bila kutetereka wakati huu mizozo ikishamiri – UN
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto kwenye mizozo Najat Maalla M’jid amewasilisha mbele ya Baraza Kuu la UN ripoti kuhusu watoto katika migogoro ya kivita akisema kwamba kutoka Agosti 2024 hadi julai 2025 ukiukaji mkubwa wa haki za watoto umeongezeka kote duniani.
Bi. M’jid amesema ripoti hiyo inaonesha madhara makubwa ambayo watoto wanakumbana nayo kutokana migogoro ya kivita kupitia utafiti wa takwimu na matukio ya ukiukaji wa haki za watoto, ikiwa ni pamoja na kuuwawa, kuhamiswa kwa nguvu na njaa.
Ukiukaji wa haki za watoto umefurutu ada
Ripoti inaonesha kuwa ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto umeongezeka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Inasisitiza madhara makubwa ambayo mapigano yanaendelea kuwaletea watoto, ikiashiria kushindwa kwa jamii ya kimataifa kuheshimu sheria za kibinadamu na haki za binadamu, pamoja na kupuuzwa kwa ulinzi maalum wa watoto na kuongezeka kwa migogoro ya kibinadamu.
“Watoto wanalipa gharama kubwa. Wanakumbwa na njaa, wanalazimika kukimbia makazi yao na wanauawa. Hili linaonesha umuhimu wa kuhakikisha amani ya kudumu na utulivu, ambayo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha ulinzi wa watoto,” amesema Bi. M’jid.
Wadau wa UN nao wanasaidia
Ripoti pia inaangazia juhudi za wadau mbalimbali kushirikiana ili kukomesha na kuzuia ukiukaji dhidi ya watoto. Ushirikiano na pande zinazohusika katika migogoro umezaa matunda, kama inavyoonekana kupitia kutiwa saini kwa mikataba ya kuwakabidhi watoto kwa mamlaka za kiraia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Yemen, pamoja na kuachiliwa kwa watoto nchini Afghanistan na Sudan.
Hadi sasa, zaidi ya mipango ya utekelezaji 40 imetiwa saini, na mazungumzo yamesababisha kuachiliwa kwa zaidi ya watoto 220,000 kutoka kwa majeshi na makundi yenye silaha.
Kwa kushirikiana na wadau wengine, kampeni mpya ya utetezi ilizinduliwa mwezi Machi 2025, kwa jina la ‘Prove It Matters’, ikilenga kuhamasisha jumuiya ya kimataifa kuunga mkono Mkataba wa haki za mtoto, huku sauti za watoto zikiwa kiini cha juhudi hizo.
Rasilimali zaidi zielekezwe kulinda watoto
Ripoti hiyo inaendelea kusisitiza umuhimu wa dharura wa kushughulikia hali ya watoto wanaoathiriwa na migogoro ya kivita. Katika kipindi hiki cha mahitaji makubwa ya kibinadamu na ulinzi wa watoto, rasilimali kwa ajili ya ulinzi wa watoto lazima ziendelee kuwepo na kuongezwa, alisisitiza Mwakilishi Maalum.
Amekumbusha kuwa, “tunapokaribia kuadhimisha miaka 30 ya tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo ya kivita, ni muhimu kuendeleza jukumu hili kwa nguvu zaidi ili kujenga juu kazi yake ya muda mrefu ya kuhakikisha ulinzi wa watoto.
“Jumuiya ya kimataifa lazima ijitolee tena na kusimamia ulinzi wa watoto. Kuwalinda watoto kunasaidia kuvunja mzunguko wa migogoro na ghasia, na kuchangia katika kuleta amani endelevu,” ametamatisha.