Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Christian Saunders azuru Tanzania kujionea maandalizi ya vikosi vya ulinzi wa amani

Christian Saunders akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika UMOJA WA MATAIFA.
UN Photo/Rick Bajornas Mratibu Maalum wa Kuboresha Hatua za Umoja wa Mataifa dhidi ya Unyanyasaji wa kingono (SEA) Christian Saunders.

Christian Saunders azuru Tanzania kujionea maandalizi ya vikosi vya ulinzi wa amani

Amani na Usalama

Mratibu Maalum wa Kuboresha Hatua za Umoja wa Mataifa dhidi ya Unyanyasaji wa kingono (SEA) Christian Saunders amefanya ziara nchini Tanzania kuona maandalizi ya vikosi vya operesheni za ulinzi wa amani katika maeneo mbalimbali duniani. 

Bendi ya jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ ikiongoza askari wengine kumkaribisha Bwana Christian Saunders hapa katika Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC) Kunduchi, Dar es Salaam.
 
Miongoni mwa askari hawa tayari wameandaliwa kwenda katika nchi mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati na hata nje ili kuusaidia Umoja wa Mataifa kutekeleza moja ya majukumu yake kwa ulimwengu, kuleta na kuitunza amani.
 
Bwana Saunders anasema, “wacha nianze kwa kusema asante. Kusema asante ni jambo muhimu sana, kwa sababu mko tayari kuanza jukumu la kutumwa, iwe mnaenda Lebanon au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au kwingineko. Mkiwa mbali na familia zenu, mbali na nchi yenu, katika mazingira yenye changamoto, na wakati mwingine katika hali hatarishi.”
 
Anawapa moyo zaidi askari lakini akiwakumbusha kuwa wao ni kioo cha ulimwengu wazingatie maadili, “na tunathamini sana kujitolea kwenu. Tunathamini sana kwamba mnaenda kuwasaidia ndugu zenu katika nchi nyingine, iwe ni nchi jirani au sehemu iliyo mbali. Mnapokwenda, mnaliwakilisha dunia. Mnawakilisha watu wa dunia.”
 
Brigedia Jenerali George Itang'are wa Chuo cha Kulinda Amani cha Tanzania ameketi kwenye kiti mbele ya Mtanzania na bendera UN .
UN News
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are akamthibitishia mgeni kwamba askari hawa wameiva na hakuna kisingizio chochote cha kutozingatia maadili huko wameandako, kisha akawahoji askari kama wanakualiana naye nao wanajibu, “twende pamoja, turudi pamoja.”