Katibu Mkuu na mashirika ya UN Walaani mashambulizi yanayohatarisha kituo cha matibabu cha Nasser Gaza
Katibu Mkuu na mashirika ya UN Walaani mashambulizi yanayohatarisha kituo cha matibabu cha Nasser Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kusaidia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) wamelaani mashambulizi ya anga kwenye Kituo cha Matibabu cha Nasser, Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel yaliyosababisha vifo vya takribani watu 20, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari watano, leo Jumatatu asubuhi ya Agosti 25.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu Guterres ameeleza tukio hilo kama ukumbusho wa hatari kubwa zinazowakabili wahudumu wa afya na waandishi wa habari katika mzozo unaoendelea.
“Mauaji haya ya kikatili yanaonesha hatari kubwa ambazo wahudumu wa afya na waandishi wa habari wanakabiliana nazo wanapotekeleza kazi zao muhimu katikati ya mgogoro huu wa kikatili,” taarifa hiyo imesema.
Bwana Guterres amesisitiza kuwa raia, wakiwemo wahudumu wa afya na waandishi wa habari, lazima waheshimiwe na kulindwa wakati wote, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Ametoa wito wa kufanyika kwa “uchunguzi wa haraka na usioegemea upande wowote” kuhusu vifo hivyo.
Aidha, amesisitiza kuwa wahudumu wa afya na waandishi wa habari lazima waweze kutekeleza majukumu yao “bila kuingiliwa, kutishwa au kudhurika.”
Akirudia wito wake wa mara kwa mara, Katibu Mkuu ametaka tena usitishaji wa mapigano wa haraka na wa kudumu, upatikanaji kamili wa misaada ya kibinadamu kote Gaza, na kuachiliwa mara moja bila masharti kwa mateka wote.
Shambulio katika Hospitali ya Nasser ni tukio la karibuni zaidi miongoni mwa mashambulizi yaliyodhoofisha mfumo wa afya wa Gaza na kuwaacha wahudumu wa mstari wa mbele wakiwa hatarini zaidi.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipoulizwa na mmoja wa waandishi wa Habari katika mkutano wa waandishi wa Habari jijini New York Marekani kuhusu kauli ya Katibu Mkuu kwa Serikali ya Israeli inapoanza shambulio jipya la kijeshi kuchukua Jiji la Gaza ni upi? Amesema, “Simamisheni. Tumekuwa wazi kabisa kuhusu madhila makubwa ambayo shambulio jipya la kijeshi dhidi ya Jiji la Gaza linaweza kuwaletea Wapalestina waliotafuta usalama huko. Hakuna sehemu salama tena iliyosalia Gaza. Tunataka kuona usitishaji wa mapigano. Tunataka kuona mateka wote wakiachiliwa huru. Tunataka kuona msaada wa kibinadamu ukirudi kuingia...”