Miaka 8 baada ya kufurushwa hali ya Warohingya inazidi kuzorota
Miaka 8 baada ya kufurushwa hali ya Warohingya inazidi kuzorota
Haki za binadamu
Leo Agosti 25 ni miaka minane tangu kufurushwa kwa wingi watu wa Rohingya kuondoka katika Jimbo la Rakhine, Myanmar.
Umoja wa Mataifa unatoa wito wa mshikamano wa kimataifa kuwasaidia kwani mateso kwa watu hao yanaendelea kuwa mabaya zaidi. Anold Kayanda na tarifa zaidi.
Myanmar (zamani ikiitwa Burma) ni nchi ya Kusini Mashariki mwa Asia yenye zaidi ya makabila 100, inayopakana na India, Bangladesh, China, Laos na Thailand.
Warohingya wanafurushwa na kuteswa kwasababu mbalimbali zikiwemo za kihistoria kwa madai kuwa walitoka Bangladesh ingawa wameishi vizazi na vizazi nchini Myanmar.
Pia sababu ya imani yao kwa uislamu miongoni mwa sababu nyingine. Ni miaka minane sasa tangu ufurushwaji mkubwa wa jami hii kutoka jimbo la Rakhine pwani ya Magharibi mwa Myanmar.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaonya kuwa Warohingya na raia wengine bado wanakabiliwa na ukiukaji wa haki za binadamu na kufurushwa.
Anaeleza wasiwasi wake kuhusu tarifa za kufukuzwa na kupunguzwa kwa nafasi za hifadhi katika ukanda huo, huku wakimbizi walioko Bangladesh wakikabiliana na upungufu mkubwa wa msaada wa chakula, elimu na huduma za afya.
Guterres anasisitiza tena wito wake wa kulindwa kwa raia wote kwa mujibu wa sheria za kimataifa na anataka mshikamano mkubwa wa kimataifa.
Hata hivyo ana matumaini kuwa Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Rohingya utakaofanyika New York mwezi ujao utasaidia kupata suluhu za kudumu.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, anaeleza kuwa jeshi la Myanmar na Jeshi la Rakhine bado wanaendeleza uhalifu mkubwa dhidi ya Rohingya bila kuchukuliwa hatua, kinyume na sheria za kimataifa na maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki na anatoa wito wa kukomesha matendo hayo ili kuvunja mzunguko wa vurugu