Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kidiplomasia kusaidia DRC zakinzana na ukatili unaoendelea

Mwanamke na watoto wawili wadogo wamepigwa picha mbele ya makazi ya muda huko Goma, DR Congo. Watoto wameshikilia kaseti za mduara wa mkono wa kati (MUAC) zinazotumika kupima utapiamlo.
© UNICEF/Esther Ushindi Watoto wengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wana utapiamlo kwa vile hawapati chakula cha kutosha.

Hatua za kidiplomasia kusaidia DRC zakinzana na ukatili unaoendelea

Amani na Usalama

Mikataba ya amani iliyofikiwa huko Washington nchini Marekani na Doha nchini Qatar ilileta matumaini ya hatua mpya katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Lakini wakati mawaziri wa mambo ya nje na wapatanishi wakiongeza idadi ya saini na mifumo ya ufuatiliaji, ghasia zinaendelea kumwaga damu katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York Marekani Martha Pobee ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya Afrika, amewaambia wajumbe wa baraza hilo “Kwa bahati mbaya, hali ya usalama inayoendelea nchini DRC haiakisi maendeleo yaliyopatikana katika uwanja wa diplomasia,”

Akifafanua zaidi ameeleza “Idadi ya vifo vya raia imeongezeka kwa kasi. Wahudumu wa kibinadamu wanaweka maisha yao hatarini kutoa msaada mdogo kwa watu ambao mahitaji yao yanaongezeka kila siku.”

Hali halisi

Jimboni Kivu Kaskazini, waasi wa M23 wanaoungwa mkono na baadhi ya askari wa Rwanda, wameendelea kutanua maeneo yao tangu wachukue mji mkuu wa jimbo hilo, Goma, Januari.

Kati ya Julai 9 na 21 pekee, zaidi ya raia 300 waliuawa, vijiji kuchomwa moto na vituo vya afya kuharibiwa.

Jimbo la Ituri nalo halijasalimika; mashambulizi ya kundi la ADF na mapigano ya makundi ya kijamii yameua makumi ya watu na kusababisha maelfu kukimbia.

Hali hii imesababisha janga kubwa la kibinadamu. Zaidi ya watu milioni sita wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku njaa na watoto wakikosa fursa ya kwenda shuleni.

Diplomasia inaendelea

Diplomasia inaendelea kupitia ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Afrika. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema mazungumzo pekee hayatoshi bila usitishaji mapigano wa dhati.

Kwa mujibu wa Bi. Pobee, “hatupaswi kukubali mateso ya kupindukia na mauaji ya mara kwa mara kuwa jambo la kawaida Mashariki mwa Congo.”

Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa kwa nia ya kweli ya pande husika na mshikamano wa jumuiya ya kimataifa, amani bado inawezekana.