Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yaonya juu ya baa la njaa lililotangazwa Gaza, yadai usitishaji haraka mapigano

Mama Mpalestina na watoto wake wanne wadogo wamekaa pamoja katika makazi ya mahema katika Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Mohammed Nateel Mwanamke akiwa na watoto wake kaskazini mwa Gaza anasema "maisha ya hapa ni magumu na ya kusikitisha."

Mashirika ya UN yaonya juu ya baa la njaa lililotangazwa Gaza, yadai usitishaji haraka mapigano

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa yametoa onyo kali leo kuhusu zaidi ya nusu milioni ya watu Gaza ambao tayari wamenaswa kwenye baa la njaa, na hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika wiki zijazo endapo hatua za dharura hazitachukuliwa.

Tathmini mpya ya  uhakika wa chakula iliyotolewa leo na IPC imethibitisha kuwepo kwa baa la njaa katika jimbo la Gaza na kutabiri kusambaa kwake hadi Deir al-Balah na Khan Younis. Shirika la Chakula na Kilimo  la Umoja wa Mataifa FAO, la kuhudumia watoto UNICEF, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO wamesema upatikanaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu ndio njia pekee ya kuzuia vifo zaidi vitakavyotokana na baa la njaa.

FAO: Chakula ni haki ya msingi ya binadamu


“Watu wa Gaza wamechoka kwa kila njia ya kuishi. Njaa na utapiamlo vinachukua maisha kila siku, na uharibifu wa mashamba, mifugo, vitalu vya mimea, uvuvi na mifumo ya uzalishaji chakula umefanya hali kuwa mbaya zaidi,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu.

Ameongeza kuwa “Kipaumbele chetu sasa lazima kiwe upatikanaji salama na endelevu wa misaada mikubwa ya chakula. Upatikanaji wa chakula siyo upendeleo ni haki ya msingi ya binadamu.”

WFP: Onyo la baa la njaa limekuwepo kwa miezi sasa
Mashirika hayo yamesema njaa lazima ikomeshwe “kwa gharama yoyote,” yakionya kwamba shambulio kubwa zaidi la kijeshi Gaza City au ongezeko la mapigano litakuwa na madhara makubwa. 

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cindy McCain, amesisitiza uharaka wa kuchukua hatua, “Onyo la baa la njaa limekuwa wazi kwa miezi kadhaa. Kinachohitajika sasa kwa dharura ni ongezeko la misaada, mazingira salama na mifumo thabiti ya usambazaji kufikia walio katika uhitaji mkubwa popote walipo”.

Amesisitiza kuwa “Upatikanaji kamili wa misaada ya kibinadamu na usitishaji mapigano sasa ni muhimu zaidi ili kuokoa maisha.”

UNICEF: Watoto wako hatarini zaidi

Watoto wamesalia kuwa kitovu cha janga hili. Utapiamlo umeongezeka kwa kasi ambayo UNICEF imeeleza kuwa ni ya maafa, huku zaidi ya watoto 12,000 wakibainika kuwa na utapiamlo mkali mwezi Julai pekee.

“Njaa sasa ni hali halisi ya kutisha kwa watoto katika mkoa wa Gaza, na tishio linalokaribia katika Deir al-Balah na Khan Younis,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell.

“Dalili zilikuwa wazi, watoto waliokonda na kuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kulia au kula, watoto wachanga wakifa kutokana na njaa na magonjwa yanayoweza kuzuilika, wazazi wakifika kliniki wakiwa hawana chochote cha kuwalisha watoto wao. Hakuna muda wa kupoteza. Bila usitishaji mapigano wa haraka na upatikanaji kamili wa fursa za misaada ya kibinadamu unahitajika, la sivyo njaa itasambaa na watoto zaidi watakufa.”ameongeza.

WHO: Baa la njaa ni janga la kutengenezwa na binadamu
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, kwa upande wake ameeleza hali hiyo kuwa ni “njaa ya kutengenezwa na binadamu” na kusisitiza hatua za haraka za kimataifa.

Amesema “Usitishaji mapigano sasa ni wajibu wa kimaadili na ni wa lazima. Utapiamlo uliosambaa unamaanisha kuwa hata magonjwa ya kawaida kama kuharisha yanakuwa hatari na kuua, hasa watoto”.

Amesisitiza kuwa “Gaza lazima ipatiwe chakula na dawa kwa haraka ili kuokoa maisha na kuanza mchakato wa kukabiliana utapiamlo. Hospitali lazima zilindwe ili ziendelee kuhudumia wagonjwa. Vizuizi vya misaada lazima vimalizike, na amani irejeshwe, ili uponyaji uanze.”