Baa la njaa kuthibitishwa Gaza Mkuu wa UN asema huku ni kushindwa kwa ubinadamu
Baa la njaa kuthibitishwa Gaza Mkuu wa UN asema huku ni kushindwa kwa ubinadamu
Zaidi ya nusu milioni ya watu huko Gaza wamekwama kwenye baa la njaa, hali iliyoghubikwa na ukosefu mkubwa wa chakula, umasikini uliokithiri na vifo vinavyoweza kuzuilika, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo ya uhakika wa chakula iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema matokeo ya uchambuzi wa Mfumo wa Hatua za Uhakika wa Chakula (IPC) si fumbo “Hili ni janga lililosababishwa na mwanadamu, shutuma ya kimaadili na ni kushindwa kwa ubinadamu wenyewe. Baa la njaa si suala la chakula, ni kuangushwa kwa makusudi kwa mifumo inayohitajika kwa ajili ya uhai wa binadamu.”
Kwa mujibu wa IPC, hali ya baa la njaa inatarajiwa kusambaa kutoka jimbo la Gaza hadi Deir Al Balah na Khan Younis katika wiki zijazo. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakionya mara kwa mara kuhusu ulazima wa kupeleka msaada wa kibinadamu kwa haraka na kwa kiwango kikubwa kutokana na kuongezeka kwa vifo vinavyohusiana na njaa, viwango vinavyozidi kuwa vibaya vya utapiamlo mkali, na kushuka kwa matumizi ya chakula huku mamia ya maelfu ya watu wakipitisha siku bila kupata chochote cha kula.
Wajibu wa Israel
“Kwa kuwa ni nguvu inayokalia kwa mabavu, Israel ina wajibu usiopingika chini ya sheria za kimataifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa chakula na vifaa vya matibabu kwa wakazi,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akirejea tamko la baa la njaa kutoka IPC, ambalo limeidhinishwa na serikali nyingi, mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi zisizo za kiserikali kama kipimo cha msingi cha uhakika wa chakula na utapiamlo.
Bwana Guterres amesema kukanusha kwa Israel wajibu wake hakutakubaliwa kuendelea, “Hakuna visingizio tena. Wakati wa kuchukua hatua si kesho ni sasa.”
Kunyamazisha mtutu wa bunduki, kuachilia mateka
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi Gaza yaliungana na Katibu Mkuu kutaka usitishaji mapigano wa haraka ili kuruhusu msaada wa kibinadamu kufikishwa bila vizuizi na kwa kiwango kikubwa, pamoja na kuachiliwa mara moja kwa mateka wote waliotekwa na Hamas na makundi mengine wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya 7 Oktoba 2023.
Mashirika hayo pia yameeleza wasiwasi mkubwa juu ya tishio la mashambulizi makali zaidi ya kijeshi dhidi ya Jiji la Gaza na uwezekano wa kuongezeka kwa mapigano, hali ambayo itakuwa na madhara zaidi kwa raia walioko tayari kwenye mazingira ya njaa.
“Watu wengi hasa watoto wagonjwa na waliodhoofika kwa utapiamlo, wazee na watu wenye ulemavu huenda wakashindwa kuondoka,” yamesema mashirika hayo katika taarifa ya pamoja.
Njaa kuenea zaidi
Ifikapo mwishoni mwa Septemba, zaidi ya watu 640,000 watakabiliwa na viwango vya hatari zaidi vya ukosefu wa chakula ambavi ni viwango vya IPC daraj la 5 katika Ukanda wote wa Gaza. Watu wengine milioni 1.14 watakuwa kwenye Daraja la 4 huku watu 396,000 zaidi wakikabiliwa na hali ya mgogoro wa chakula wa Daraja la 3.
Hali Kaskazini mwa Gaza inakadiriwa kuwa mbaya sawa au zaidi kuliko Gaza City. Hata hivyo, ukosefu wa takwimu kamili ulizuia uainishaji wa IPC, jambo linaloonesha ulazima wa kupata fursa ya ufikiaji.
Uainishaji wa njaa unamaanisha viwango vikali zaidi vinavyochochewa pale viwango vitatu vya msingi ambavyo ni ukosefu mkubwa wa chakula, utapiamlo mkali na vifo vinavyohusiana na njaa vinapovukwa.
Uchambuzi wa hivi karibuni sasa unathibitisha kwa ushahidi wa kuridhisha kuwa vigezo hivi vimetimia, kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Akiwafahamisha waandishi wa habari leo Ijumaa mjini Geneva, Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amesema ni njaa ambayo ingeweza kuzuilika “kama tungepewa ruhusa.”
Njaa katika ardhi yenye rutuba
“Lakini chakula kimekwama mipakani kwa sababu ya vizuizi vya kimfumo vinavyowekwa na Israel. Ni njaa ndani ya mamia machache ya mita kutoka kilipo chakula, katika ardhi yenye rutuba. Ni njaa tuliyoitolea onyo mara kwa mara lakini vyombo vya habari vya kimataifa havijaruhusiwa kuingia kuripoti na kushuhudia,” ameongeza Fletcher .
Ameendelea kusema kuwa “Ni njaa ya mwaka 2025. Njaa ya karne ya 21 ikishuhudiwa na Ndege siziso na rubani au droni na teknolojia ya kijeshi ya hali ya juu zaidi katika historia. Ni njaa ambayo viongozi fulani wa Israel wameitumia waziwazi kama silaha ya vita.”
Kwa upana zaidi, Bwana Fletcher amesema, “hii ni njaa ya dunia. Ni njaa inayouliza, ‘ulifanya nini?’ Njaa ambayo italitesa taifa hilo na lazima itutese sote.”
Mashirika ya Umoha wa Mataifa yamesema utapiamlo miongoni mwa watoto huko Gaza unaongezeka kwa kasi ya kutisha yakibainisha kwamba mwezi Julai pekee, zaidi ya watoto 12,000 waligunduliwa kuwa na utapiamlo mkali idadi ya juu zaidi iliyowahi kurekodiwa kwa mwezi mmoja na ongezeko la mara sita tangu mwanzo wa mwaka.
Baa la njaa la kwanza Mashariki ya Kati
Tangu uchambuzi wa mwisho wa IPC mwezi Mei, idadi ya watoto wanaotarajiwa kuwa kwenye hatari kubwa ya kifo kutokana na utapiamlo kufikia mwishoni mwa Juni 2026 imeongezeka mara tatu kutoka 14,100 hadi 43,400.
Tathmini mpya inaripoti kuzorota kwa kiwango kikubwa zaidi tangu IPC ianze kuchambua uhakika wa chakula na utapiamlo mkali katika Ukanda wa Gaza, na inaashiria mara ya kwanza baa la njaa limethibitishwa rasmi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Tangu mwezi Julai, usambazaji wa chakula na misaada kuingia Gaza umeongezeka kidogo lakini umesalia kuwa mdogo sana, usio wa kudumu na usioweza kufikiwa kwa mahitaji halisi.
Wakati huo huo, takribani asilimia 98 ya mashamba katika eneo hilo yameharibiwa au hayafikiki jambo lililoimaliza sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula wa ndani na watu tisa kati ya kumi wamelazimika kukimbia makazi yao mara kwa mara.
Baa hili la njaa linaweza kuwa uhalifu wa kivita: OHCHR
Akitoa kauli yake kuhusu kuthibitishwa kwa baa hilo la njaa Gaza Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema baa hili la njaa ni “matokeo ya moja kwa moja ya sera za Serikali ya Israel”.
Ameendelea kusema kuwa , “Ni uhalifu wa kivita kutumia njaa kama mbinu ya vita, na vifo vinavyotokana na hilo pia vinaweza kuhesabiwa kama uhalifu wa kivita wa mauaji ya makusudi.”
Türk ameongeza kuwa “Mamlaka za Israel lazima zichukue hatua za haraka kukomesha baa la njaa katika jimbo la Gaza na kuzuia vifo zaidi kote Ukanda wa Gaza. Lazima zihakikishe kuingia kwa msaada wa kibinadamu mara moja, kwa kiwango cha kutosha, na kutoa fursa kamili kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na ya kibinadamu mengine kutekeleza wajibu wao.”