Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM na AU wakubaliana kuimarisha usimamizi wa wahamiaji barani Afrika

Wahamiaji wa Afrika Mashariki waliojaribu kuvuka bahari ya Mediterania wanaokolewa na jeshi la wanamaji la Italia huko Sicily.
© UNICEF/Gideon Mendel Wahamiaji wa Afrika Mashariki waliojaribu kuvuka bahari ya Mediterania wanaokolewa na jeshi la wanamaji la Italia huko Sicily.

IOM na AU wakubaliana kuimarisha usimamizi wa wahamiaji barani Afrika

Wahamiaji na Wakimbizi

 Shirika la umoja wa mataifa la uhamiaji IOM na Muungano wa Afrika AU wameingia makubaliano mapya ya kushirikiana kimkakati katika kuimarisha namna ya kushughulikia wahamiaji barani Afrika kupitia mkataba mpya wa miaka mitatu uliosainiwa na mashirika hayo jijini Yokohama nchini Japan.

Taarifa ya pamoja kutoka Yokohama Japan na Addis Abba Ethiopia imeeleza kuwa mkataba huo ni unathibitisha wa dhamira yao ya kuhakikisha uhamiaji unachangia maendeleo, uthabiti, na ustawi kote barani Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope anasema “Makubaliano haya mapya yanaonesha azimio letu la pamoja na Muungano wa Afrika ya kuweka uhamiaji katikati ya ajenda ya maendeleo ya Afrika” na kuongeza kuwa “Kwa kuimarisha mifumo ya sera, kulinda haki za wahamiaji na kuwekeza katika uhamiaji wenye staha, tunaweza kufungua fursa kwa mamilioni ya watu na kujenga mnepo. Hii sio tu katika kujenga jamii jumuishi Afrika bali pia katika kuonesha namna ambavyo uhamiaji unao simamiwa vyema unavyoweza kunufaisha nchi walizotoka, wanapopita na walipofikia.”

Mkataba huu unaendeleza makubaliano ya ushirikiano ulioanzishwa mwaka 2022, na unaonesha maono ya pamoja ya kutumia uhamiaji kama kichocheo cha ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu. Unatoa mwelekeo wa ushirikiano baina ya IOM na AU, kuhakikisha kuwa nchi wanachama wa Afrika zinapata zana na msaada wanaohitaji ili kusimamia uhamaji kulingana na vipaumbele vya bara la Afrika na ahadi za kimataifa.

Makubaliano haya mapya ya IOM na AU yanaimarisha ushirikiano kwa kuzipa kipaumbele sera za uhamiaji zinazozingatia haki za binadamu na usawa wa kijinsia, kukuza uhamaji wa kikanda na kutumia fursa za Soko Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Ushirikiano huu unaenda sanjari na utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Uhamiaji Salama na unaoangazia ulinzi wa haki za wahamiaji.

Soma zaidi kuhusu makubaliano hayo hapa