Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali ya kisiasa na kibinadamu Syria

Mtazamo wa Baraza la Usalama wakati wa kikao kuhusu Syria
UN Photo/Evan Schneider
Mtazamo wa Baraza la Usalama wakati wa kikao kuhusu Syria

Baraza la Usalama lajadili hali ya kisiasa na kibinadamu Syria

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekutana mjini New York Marekani  kumejadili hali ya kisiasa na kibinadamu nchini Syria, ambapo limepokea taarifa kutoka kwa Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa Syria Geir O Pedersen na Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher.

Mkutano huo umejikita kwenye kusuasua kwa usitishaji mapigano mjini Sweida na changamoto kubwa zaidi za mchakato wa kisiasa nchini Syria.

Usitishaji mapigano wakubwa na changamoto

Akitoa tarifa yake mbele ya wajumbe wa Baraza hilo Mjumbe Maalum Pedersen ameonya kwamba usitishaji mapigano uliokubaliwa Sweida tarehe 19 Julai “umekabiliwa na changamoto kubwa,” akibainisha kwamba vurugu zinaweza kuibuka tena wakati wowote. “Nchi bado ni dhaifu sana, na kipindi cha mpito kiko katika hatihati kubwa” amewaambia wajumbe wa Baraza.

Amesisitiza kwamba bila hatua madhubuti za kujenga imani, mapatano hayo yanaweza kubaki kuwa “mapumziko ya muda badala ya msingi wa uthabiti wa kudumu.”

Mji wa Sweida Magharibi mwa Syria
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman
Mji wa Sweida Magharibi mwa Syria

Hali ya kisiasa yazorota

Pedersen ameeleza wasiwasi kwamba mwezi mmoja wa “utulivu wa kijeshi umekuwa ukificha mvutano wa kisiasa unaozidi kuongezeka, ikiwemo ongezeko la misimamo mikali na siasa za ushindi au kushindwa”.

Amebainisha kuwa kuundwa kwa kamati ya utawala wa ndani Sweida na baadhi ya wito wa msaada kutoka nje kumezua tuhuma za nia za kujitenga.

Amesisitiza kuwa “Vyombo vya usalama vya mamlaka za mpito lazima vioneshe wazi kwamba vinachukua hatua kulinda Wasyria wote na si tishio kwao”.

Wito wa mpito jumuishi

Akiangazia maandalizi ya uchaguzi wa moja kwa moja kwa ajili ya Bunge la Mpito la Watu, Pedersen amesisitiza kuwa Wasyria wanapaswa kuona mchakato wa mpito kama “njia iliyo wazi na jumuishi kuelekea amani, si mlolongo wa makubaliano ya muda mfupi”. Pedersen amewataka viongozi wa mpito kuwa na uongozi thabiti, ujasiri wa kufanya maridhiano na kuzingatia utawala wa sheria, akinukuu maneno ya Rais wa Mpito Sharaa amesema “Umoja haujengwi kwa nguvu na damu, bali kwa kuelewana na mazungumzo.”

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama
UN Photo/Loey Felipe
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama

Hali ya kibinadamu bado mbaya: OCHA

Kati ya hali tete ya kijeshi na kisiasa, Waasiriya milioni 16 kote nchini wanahitaji msaada wa kibinadamu, kulingana na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher.

Zaidi ya hayo, watu zaidi ya 185,000 wamehama kutoka makazi yao katika mikoa ya Sweida, Dar’a, Damascus vijijini na maeneo mengine.

“Hali kwa ujumla ni mbaya. Tunahitaji kuendeleza usambazaji wa dharura wa chakula, huduma za afya, makazi, maji safi, mafuta, urejeshaji wa miundombinu ya maji na umeme, na elimu. Katika baadhi ya maeneo, idadi ya watu wanaoingia sasa ni kubwa kuliko idadi ya wakazi waliokuwepo. Huduma ziko chini ya shinikizo kubwa,” amesema Bwana Fletcher.

Timu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Msaada wa Kibinadamu (OCHA) zimetembelea Sweida na miji mingine, zikisambaza msaada na kutathmini mahitaji.

OCHA pia imetoa vifurushi vya chakula cha dharura, unga na bidhaa muhimu za kaya kwa maelfu ya watu.

Hata hivyo, ukosefu wa usalama na kufungwa kwa barabara kumeathiri usambazaji wa msaada kutoka Umoja wa Mataifa, washirika wa NGO na Chama cha Msalaba Mwekundu Syria.

“Tunahitaji upatikanaji bora wa fursa za ufikiaji wa kibinadamu na kibiashara. Na zaidi ya yote, tunahitaji usalama,” amesisitiza Bwana Fletcher, akirejelea hasa mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada, vituo vya afya, wauguzi na magari ya wagonjwa.

Watu wakipita kwenye mitaa ya jimbo la As-Sweida Syria
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman
Watu wakipita kwenye mitaa ya jimbo la As-Sweida Syria

Ufadhili finyu wapunguza misaada ya kibinadamu

Hata hivyo, “pamoja na changamoto za fedha na usalama, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha kadri tuwezavyo kwa rasilimali tulizo nazo,” wakifikia watu milioni 3.5 kwa wastani kila mwezi, ongezeko dhahiri kutoka mwaka uliopita.

Lakini kwa kuwa ombi la kibinadamu la 2025 nchini Syria limefadhiliwa kwa asilimia 14 pekee, upunguzaji wa msaada unaoendelea katika miji mingi ya Magharibi unatarajiwa kusababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi angalau asilimia 40 katika jamii ya kibinadamu ndani ya Syria.

Kiongozi huyo wa misaada wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba bila fedha zaidi, “hatutaweza kudumisha juhudi hizi muhimu, achilia mbali kuzifikisha kwa wingi kwa watu zaidi wanaohitaji msaada.”

Zaidi ya hayo, ingawa amehimiza msaada wa kibinadamu, pia amesisitiza kuwa uwekezaji wa maendeleo ya muda mrefu unahitajika nchini Syria ili “kupunguza na hatimaye kuisha utegemezi wa msaada wa kibinadamu.”