Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu mkubwa wa unaendelea Gaza, Mkuu wa UN arejea wito wa kusitishwa mapigano

Wanaume na wavulana wakiwa wameshikilia vyungu na vyungu juu ya uzio wa chuma huku wakisubiri chakula katika jiko la jamii magharibi mwa Jiji la Gaza.
UN News Watu wa Gaza wakisubiri chakula kwenye jiko la jamii Gaza City

Uharibifu mkubwa wa unaendelea Gaza, Mkuu wa UN arejea wito wa kusitishwa mapigano

Amani na Usalama

Wakati operesheni za kijeshi za Israel zikidaiwa kuendelea kuongezeka ndani na kuzunguka Jiji la Gaza leo Alhamisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerejelea wito wake wa dharura wa kusitishwa kwa mapigano, huku Wapalestina wakikimbia mashambulizi makali ya anga, makombora na risasi.

“Ni muhimu kufikia haraka makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza,” Katibu Mkuu aliwaambia waandishi wa habari kando ya Mkutano wa Tisa wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD9) unaofanyik jiji Tokyo Japan, na kutaka “ kuachiliwa mara moja bila masharti yoyote mateka, pamoja na kuepusha vifo na uharibifu mkubwa ambao mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Jiji la Gaza yatasababishaa.”

Takribani watu milioni moja bado wanaishi katika jiji hilo kubwa zaidi la Gaza Kaskazini  lililokumbwa na vita.

Jeshi la Israel limekuwa likilieleza eneo hilo kama ngome ya Hamas, kundi linaloelezwa kuwa la kigaidi ambalo mashambulizi yake ya kikatili nchini Israel na utekwaji mateka wa watu ulizua vita mnamo 7 Oktoba 2023.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amelaani uamuzi wa Serikali ya Israel wa kuidhinisha mpango wa muda mrefu wa kupanua makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

“Uamuzi wa mamlaka za Israel kupanua ujenzi wa makazi haramu, jambo litakalogawanya Ukingo wa Magharibi, lazima ubatilishwe. Ujenzi wowote wa makazi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa,” amesisitiza.

Makazi hayo yanadaiwa kupewa ruhusa ya kujenga zaidi ya nyumba 3,000, shule na zahanati, hatua ambayo itakata kabisa Jerusalem Mashariki kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, eneo lililotwaliwa na Israel katika Vita vya Siku Sita mwaka 1967 baada ya kuishinda Misri, Jordan na Syria.

Mwanamke aliyevaa jina la Shirika la Afya la Dunia amesimama nyuma ya kamera, akitazama jengo lililoharibiwa huko Gaza.
© WHO Mfanyakazi wa WHO akitathimini uharibifu wa hospitali Kaskazini mwa Gaza

Uharibifu mkubwa mijini

Katika taarifa yake kuhusu Gaza, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imebainisha kuwa jeshi la Israel lilitangaza tarehe 20 Agosti kuwa “hatua ya awali ya operesheni dhidi ya Jiji la Gaza ilikuwa imeanza, likilenga Jabalya kaskazini mwa Gaza na Az Zaytoun jijini Gaza”.

OHCHR imeripoti mashambulizi makali na yanayoendelea ya kijeshi ya Israel yaliyolenga Jabalya Al Balad na Jabalya Al Nazla, na pia mashambulizi mengine dhidi ya watu waliokuwa wakitafuta misaada eneo la Zikim.

“Mashambulizi ya angani, mizinga na mabomu ya ndege zisizo na rubani yameendelea kuripotiwa, ikiwemo dhidi ya majengo ya makazi,” imesema ofisi hiyo ya haki za binadamu, huku kukiwa na ripoti za nyumba kuharibiwa Jabalya kwa mabomu.

Mlipuko mkubwa uliteketeza jengo katika Ukanda wa Gaza, na kusababisha moto mkubwa na moshi dhidi ya anga lenye giza.
© UNRWA/Ashraf Amra Mashambulizi ya anga yaharibu majengo katika Ukanda wa Gaza.

Maonyo kupitia ndege ndogo zisizo na rubani

Jeshi la Israel pia linaripotiwa kuendelea kutoa amri za watu kuhamishwa kupitia quadcopters ambazo ni ndege ndogo zisizo na rubani na pia simu za moja kwa moja kwa wakazi wa maeneo makubwa ya Jabalya, kwa mujibu wa OHCHR.

Wakati huo huo ndani ya Jiji la Gaza, maeneo yote ya mijini yamekuwa yakiharibiwa kabisa, Umoja wa Mataifa unaeleza, huku uharibifu zaidi ukiendelea kusini na kusini mashariki kadri operesheni za kijeshi zinavyoendelea.

Mashambulizi ya karibuni yamekuwa mabaya zaidi hasa katika vitongoji vya Az Zaytoun na As Sabra. Pia, mashambulizi ya angani yametajwa kulenga majengo ya makazi au mahema ya wakimbizi huko Ash Sheikh Radwan, Ash Shujaiyeh na Kambi ya Ash Shati, na kusababisha vifo vingi, kwa mujibu wa OHCHR.

Kumefanyika zaidi ya mashambulizi 50 dhidi ya majengo ya makazi na vitalu vyote vya nyumba jijini Gaza tangu 8 Agosti huku OHCHR ikionya jana Jumatano kuwa “uharibifu wa kimfumo wa jiji la Gaza umeanza.”

“Familia kadhaa zinaripotiwa kunaswa kutokana na mabomu yanayoendelea kurushwa,” imesema OHCHR ikinukuu ripoti kuwa ubomoaji mkubwa wa majengo unaendelea Gaza Kaskazini na Mashariki.

Aidha, uhamaji mkubwa wa watu umeripotiwa kutoka Gaza Kaskazini na Jiji la Gaza kuelekea magharibi mwa jiji, ingawa takwimu bado hazijapatikana.

Mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya mahema yaliyowahifadhi watu katika eneo la Al Mawasi, magharibi mwa Khan Younis, pia yameripotiwa, imeongeza ofisi ya OHCHR.

Mwanamke aliyevaa hijab anamhudumia msichana mdogo mwenye utapiamlo mkali katika mazingira ya kliniki.
© WHO Msichana aliyedhoofika sana kwa utapiamlo huko Gaza. Mashirika ya misaada yamekuwa yakiitaka Israel mara kwa mara iruhusu misaada zaidi kuingia Gaza ili kuzuia janga la kibinadamu linaloendelea.

Utapiamlo mkali wakithiri

Wakati huohuo, timu za misaada za Umoja wa Mataifa zimebainisha athari mbaya ya operesheni inayoendelea ya kijeshi ya Israel, ambapo viwango vya utapiamlo mkali miongoni mwa watoto jijini Gaza vimepanda hadi asilimia 28.5 ambayo ni zaidi ya mtoto mmoja kati ya wanne.

“Watoto wanaendelea kufa kutokana na njaa inayosababishwa na binadamu,” limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kwenye taarifa yake leo, ikibainisha kuwa tangu Machi 2025, baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuvunjika, imewapima zaidi ya watoto 95,000 wenye umri wa miezi sita hadi miaka mitano kwa utapiamlo katika Ukanda mzima wa Gaza.

Wakati makubaliano ya kusitisha mapigano yalipodumu mapema Machi na misaada iliruhusiwa kuingia Gaza kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko sasa, viwango vya utapiamlo jijini Gaza vilikuwa chini mara sita, yaani asilimia 4.5 pekee, kulingana na UNRWA.

Kwa Gaza yote, utapiamlo mkali ulipanda hadi karibu asilimia 16 katikati ya mwezi Agosti, zaidi ya mara tatu juu ya kiwango cha asilimia 5.2 kilichorekodiwa na UNRWA mwezi Machi.

Watoto wa Kipalestina wakikusanya maji kwenye makopo katika kitongoji cha Al-Shaboura huko Rafah, Gaza.
UN News/Ziad Taleb WAtoto wakijaza maji ya kunywa kwenye madumu huko kitongoji cha Al-Shaboura, eneo la Rafah, kusini mwa Gaza

Huduma muhimu zipo hatarini

Kwa sasa, huduma zinazotolewa na UNRWA katika Jiji la Gaza ziko “katika hatari kubwa,” shirika hilo limeonya, likibainisha kuhusu maelfu kwa maelfu ya watu wanaoishi katika makao yake ya muda na “wengi zaidi waliobaki maeneo ya jirani.

Kuna wasiwasi mkubwa kuhusu ofisi kuu ya UNRWA ya uga wa Gaza kitovu chake kikubwa cha vifaa kaskazini mwa Gaza kwani shughuli za shirika hilo kusini “zimelemazwa na amri za kuhamishwa na mashambulizi ya mabomu”.

Kama ishara ya jukumu muhimu la UNRWA katika utoaji misaada Gaza, imebainisha kuwa mwezi uliopita pekee, ilitoa mashauriano ya kitabibu zaidi ya 100,000 na kupima watoto 3,500 kwa utapiamlo jijini Gaza.

UNRWA pia ilisambaza maji ya kunywa kwa watu 220,000, maji ya matumizi ya nyumbani kwa watu 250,000 na kuondoa mamia ya tani za taka.

Wataalamu wa elimu na ulinzi wa shirika hilo walifikia maelfu zaidi ya watu katika maeneo ya kujifunza ya muda au kwa kutoa ushauri, shughuli za burudani na mafunzo ya uelewa kuhusu hatari za mabaki ya silaha hatari.

“Wakati wenzetu, kama walivyo wafanyakazi wengine wa Umoja wa Mataifa, wameamua kubaki na kuendelea kutoa huduma, huduma hizi zote sasa ziko hatarini kutokana na operesheni kali za kijeshi,” imeonya UNRWA .