Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atanabaisha vipaumbele vitano kwa maendeleo ya Afrika

Katibu Mkuu UN Antonio Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa TICAD 9 mjini Yokohama, Japan, mwaka 2025.
UN Photo/Ichiro Mae Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika, Yokohama, Tokyo 20 Agosti 2025.

Katibu Mkuu wa UN atanabaisha vipaumbele vitano kwa maendeleo ya Afrika

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesisitiza haja ya mageuzi ya muda mrefu ya Baraza la Usalama na mfumo wa kifedha wa kimataifa ili Afrika ipate uwakilishi wenye nguvu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amefafanua vipaumbele hivyo vitano vya kusongesha mbele maendeleo ya Afrika na nafasi yake duniani:

Mosi ni mageuzi ya utawala wa dunia: Akihutubia leo kwenye Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Maendeleo ya Afrika TICAD IX jijini Tokyo Japan Guterres ametoa wito wa mageuzi ya muda mrefu yanayohitajika katika Baraza la Usalama na mabadiliko ya mfumo wa kifedha wa kimataifa ili Afrika ipate uwakilishi wenye nguvu zaidi.

Amesisitiza msamaha wa madeni, akibainisha kuwa nchi 34 zinatumia fedha zaidi kulipa madeni kuliko kwenye afya na elimu. Tunahitaji msamaha wa madeni na mageuzi ya haraka”. amesisitiza

Pili ni uwekezaji katika minyororo endelevu ya thamani: Guterres ameihimiza Afrika kuondokana na utegemezi wa kuuza malighafi pekee, ikiwemo madini muhimu, kwa kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani, kuunda ajira na kuimarisha mifumo ya chakula, nishati na uzalishaji.

Katibu Mkuu UN António Guterres akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengi wa Afrika katika mkutano wa TICAD 9 huko Yokohama, Japani.
UN Photo/Ichiro Mae Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, Yokohama, 20 Agosti 2025.

Akiwa na wasiwasi kwamba watu milioni 600 barani humo bado hawana nishati ya umeme, amesema ni jambo lisilo la haki kwamba Afrika inapokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa dunia katika nishati jadidifu licha ya uwezo wake mkubwa katika jua, upepo, maji na madini muhimu.

Tatu kutumia ubunifu wa kidijitali: Katibu Mkuu amesema teknolojia za kidijitali kuanzia serikali zinazotumia TEHAMA kutoa huduma au e-Government hadi huduma za kifedha kwa njia ya simu zinafungua fursa mpya, lakini Afrika bado ipo nyuma.

Guterres ametoa wito wa msaada wa kimataifa kuhakikisha kwamba Akili Mnemba AI, inachochea ukuaji jumuishi kote barani.

Nnne ni kuweka kipaumbele kwa watu: Kwa kuwa Afrika ndio nyumbani kwa idadi kubwa zaidi ya vijana duniani, Guterres amesisitiza uwekezaji mkubwa katika elimu, ujuzi, ajira na ushiriki wa wanawake.

Masuala haya, amesema, yatajadiliwa kwa upana kwenye mkutano ujao wa dunia kuhusu Maendeleo ya Kijamii utakaofanyika Doha Qatar.

Na tano ni kuunganisha amani na ustawi:  Katibu Mkuu ameoya kwamba migogoro nchini Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Somalia, Sahel na maeneo mengine bado inanyonya rasilimali na kuzuia uwekezaji.

“Maendeleo endelevu yanahitaji amani endelevu,” amesema, akitoa wito wa kuchukua hatua madhubuti zaidi “kukomesha milio ya bunduki na kukuza uthabiti".

Katika  mkutano huo Guterres aliwakumbusha wajumbe kwamba matarajio ya Afrika tayari yamewekwa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu SDG's na Ajenda 2063 ya Muungano wa Afrika, na akasisitiza kwamba ushirikiano unaooneshwa katika TICAD unaweza kuyafanya malengo haya kuwa halisi.

Amehitimisha hotuba yake kwa wito kwamba “Hebu tushirikiane kuunda suluhisho litakalojenga mustakabali wa heshima, fursa na amani kwa wote”.