Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mguu wake ulikatwa akiwa anatafuta chakula Gaza

Mwanamume Mpalestina Ibrahim Abdel Nabi ameketi katika makazi ya muda huko Gaza na watoto wake, akiangalia kiungo bandia alichotengeneza mwenyewe.
UN News Ibrahim Abdel Nabi, Mpalestina aliyekimbia makazi yake huko Gaza, akiwa ameketi na watoto wake huku akitazama kiungo cha bandia alichojitengenezea kumsaidia kusogea.

Mguu wake ulikatwa akiwa anatafuta chakula Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Miezi michache iliyopita, Mpalestina Ibrahim Abdel Nabi alitoka kwenda kupeleka msaada wa kibinadamu kwa familia yake katika Ukanda wa Gaza, lakini safari hiyo ilibadilika ghafla alipigwa risasi ya mlipuko, akapoteza mguu mmoja na kupelekwa hospitalini baada ya kuvuja damu kwa takriban saa mbili.

Ibrahim amesema  alikaa mwezi mmoja na nusu katika hospitali ya Msalaba Mwekundu karibu na eneo la Alam, magharibi mwa Rafah, kusini mwa Gaza, kabla hali yake mbaya sana kutulia. Katika hema lake kwenye kambi ya wakimbizi eneo la Mawasi, Khan Younis, kusini mwa Gaza, Ibrahim Abdel Nabi alizungumza na mwandishi wa habari wa UN mjini Gaza, huku akiangalia picha yake kwenye simu kabla ya kupoteza mguu wake mnamo Mei 27, 2025.

Mwanamume Mpalestina, Ibrahim Abdel Nabi, ameketi kwenye kiti huku mkewe akimsaidia kuvaa mguu bandia uliotengenezwa kwa mikono. Magongo yanaonekana nyuma.
UN News Ibrahim Abdel Nabi, Mpalestina aliyekimbia makazi yake huko Gaza, akiwa ameketi kwenye kiti huku mkewe akimsaidia kuvaa kiungo cha bandia kilichotengenezwa kwa mikono.

“Tuliambiwa kwamba Shirika la Misaada la Gaza limefungua milango yake kugawa msaada kupitia kadi za utambulisho. Mimi na mke wangu tulikubaliana nichukue kadi yangu niende. Nilipofika eneo la Al-Alam, magharibi mwa Rafah, kuchukua msaada, nikagongwa na risasi ya mlipuko mguuni na nikakatwa mguu papo hapo. Nilikuwa navuja damu kwa takriban saa moja na nusu, na hakuna aliyeweza kunisaidia. Kila mtu alikuwa ameshughulika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto wao.”

Lakini kikundi cha watu kilikuja kumwokoa na kumpeleka hospitali ya karibu ya Msalaba Mwekundu.

“Nilikaa pale kwa mwezi mmoja na nusu. Nilifanyiwa upasuaji kama 12, wengi wao wakiwa ni wa kusafisha vidonda. Nilidhoofika sana kwa kukosa lishe na kupoteza damu nyingi. Kila mara maambukizi yalikuwa yanasambaa kwenye miguu, na walilazimika kukata sehemu nyingine zaidi hadi kufikia hali hii.”

Mguu wa bandia alioutengeneza mwenyewe

Maumivu ya kupoteza kiungo yaliongezeka zaidi wakati watoto wake wanne walipokuwa wanakumbwa na njaa na kumuuliza awapelekee msaada kama familia nyingine. Aliongeza kusema:

Familia ya Wapalestina imeketi ndani ya hema, akiwemo baba mwenye kiungo bandia na magongo, pamoja na mke wake na watoto wanne.
UN News Ibrahim Abdel Nabi, Mpalestina aliyekimbia makazi yake huko Gaza, akiwa ameketi katika hema lake na mke wake na watoto wanne.

“Watoto wangu waliponiuliza kuhusu chakula, hali yangu ya kiakili ilizidi kuwa mbaya, na nilikuwa kwenye maumivu makali waliponiambia, ‘Baba, hatuna unga.’ Hii ilinipa motisha kutumia vifaa tulivyo navyo kutengeneza mguu wa bandia. Mimi na mke wangu tulifikiria kutengeneza mguu wa bandia kwa kutumia vifaa rahisi tulivyokuwa navyo, ili niweze kupeleka msaada na kubeba mfuko wa unga mgongoni. Angalau nitaweza kupeleka chakula na maji kwa mke na watoto wangu. Nilitengeneza huo mguu wa bandia, na Alhamdulillah niliweza kutembea nao.”

Watoto wake na mke wake walipokuwa wakimzunguka ndani ya hema la wakimbizi huku wakikumbuka walivyokutana, mkewe alimwambia kuwa kukatwa kwa mguu huo hakutabadilisha chochote, bali kumfanya kuwa mwenye nguvu zaidi na mwenye heshima kubwa. ‘Insha’Allah tutapitia kipindi hiki Pamoja.’ Alijikuta akilia kwa machozi yaliyomtiririka, lakini alisema, “Ninavumilia, Alhamdulillah.”

Ingawa mguu wa bandia alioutengeneza mwenyewe, “hauko vizuri, hauwezi hata kufidia asilimia 20 ya ulemavu wangu, wala hauwezi kuchukua nafasi ya miguu yangu, lakini angalau naweza kuutegemea kuleta chakula na maji. Nitaendelea kuutumia mguu huu hata kama unaniumiza, unaweza kunijeruhi zaidi, kusababisha uvimbe, na kuongeza maumivu. Kwa sasa hatuna huduma yoyote ya afya wala vifaa vya tiba. Hali inazidi kuwa mbaya kila siku.”

Kisha Ibrahim na mke wake walielekea kumsaidia kutembea hadi kwenye hema lililokuwa karibu, ambako alimsaidia kuvaa mguu wa bandia, akimtia moyo, na ndipo akaanza kutembea taratibu kwa kutumia mkongojo, huku mkewe akiwa anamwambia mara kwa mara: “Usijichoshe. Chukua muda wako na tembea polepole.”

Ibrahim Abdel Nabi, Mpalestina aliyehamishwa kutoka makazi yake huko Gaza, anatembea kwa kutumia mguu wake wa bandia alioutengeneza mwenyewe, huku mke wake akimsaidia.

Ibrahim Ibrahim Abdel Nabi, Mpalestina aliyehamishwa kutoka Gaza, anatembea akiwa na kiungo cha kinga kilichotengenezwa kwa mikono, akiungwa mkono na mke wake.
UN News Ibrahim Abdel Nabi, Mpalestina aliyekimbia makazi yake huko Gaza, akitembea na kiungo cha bandia kilichotengenezwa kwa mkono, akiungwa mkono na mke wake.

Alienda kununua chakula, akapoteza mguu

Gaza kwa sasa ina idadi kubwa zaidi ya watoto waliokatwa viungo kwa uwiano wa watu kuliko nchi nyingine yoyote duniani.

Katika Hospitali ya Shifa, baadhi ya watoto wanapata matibabu, wakiwemo watoto kama Shahd, ambaye alipoteza mkono wake wa kushoto kutokana na shambulio la anga la Israeli.

“Nilikuwa nimesimama mbele ya nyumba yetu wakati vipande vya bomu vilinipiga, nikajeruhiwa na kupoteza mkono wangu,” Shahd alimweleza mwandishi wetu.Shahd anatamani kupata mkono wa bandia ili aweze tena kuutumia mkono wake na kiganja.

Katika kitanda kilicho jirani, msichana mdogo Mariam analia kwa maumivu, na anampata rafiki yake amekaa naye kumfariji. Mariam alipoteza mguu mmoja, huku mguu mwingine ukiwa umejeruhiwa vibaya.

Mtoto wa Kipalestina Maryam Abu Alba amelala kwenye kitanda katika hospitali moja huko Gaza, akiwa amekatwa mguu wake wa kulia na mguu wa kushoto ukiwa umejeruhiwa vibaya.Nyanyaye Maryam alimweleza mwandishi wetu kwamba, nyumba  ya jirani yao ililipuliwa kwa bomu, halafu nyumba yao ikapigwa pia. Mguu wa Maryam ulikatwa, na mguu mwingine ukawekewa chuma kwa sababu ya kuvunjika. Anateseka sana kutokana na kukatwa kwa mguu.Aliongezea  kuomba msaada kutoka kwa yeyote yule kumpatia kiungo bandia na kumsaidia matibabu ya mguu mwingine kwa sababu mishipa na kano zimeharibiwa.

Katika hospitali hiyo hiyo, Mohammed Hassan anatazama mguu wake alioupoteza alipokuwa katika harakati za kununua chakula.

Mtoto wa Kipalestina Mohammed Hassan anakaa kwenye kitanda hospitalini Gaza baada ya kukatwa mguu wake wa kushoto kutokana na mashambulizi ya mabomu. Alisema kwa sauti yake ya kitoto:

“Nilikuwa naenda kununua falafel. Niliporudi, kabla sijafika nyumbani, nilitazama juu na kuona roketi ikianguka juu yetu. Nilijaribu kukimbia, lakini ilikuwa haraka mno. Nilijikuta nimeshikwa ukutani, na nilipotazama, mguu wangu ulikuwa umekatwa. Kisha mtu mmoja akanichukua na kunipeleka hospitali hii.”