WHO: Viboko bado vyatawala shuleni na majumbani vikiathiri watoto bilioni 1.2 duniani
WHO: Viboko bado vyatawala shuleni na majumbani vikiathiri watoto bilioni 1.2 duniani
Ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Afya Duniani WHO imebaini kuwa adhabu ya viboko bado imesambaa kwa kiwango cha kutisha, ikiwakosesha usalama na haki takribani watoto bilioni 1.2 duniani kote wanaoathiriwa majumbani mwao kila mwaka.
Utafiti wa shirika hilo uliohusisha takwimu kutoka nchi 58 umeonesha kuwa asilimia 17 ya watoto waliopigwa viboko katika mwezi uliopita walikumbwa na aina kali zaidi za adhabu hiyo ikiwa ni pamoja na kupigwa kichwani, usoni au masikioni, au kutandikwa mara nyingi kwa nguvu.
“Hii si nidhamu, ni unyanyasaji,” alisema Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa WHO anayeshughulika na sababu za kijamii za afya. Ameongea kuwa “Ushahidi uko wazi, viboko vinaharibu maendeleo ya kimwili, kihisia na kiakili ya watoto. Hakuna mtoto anayepaswa kupigwa kwa jina la kurekebishwa.”
Ripoti inasema kiwango cha matumizi ya viboko kinatofautiana sana miongoni mwa nchi. Kati ya watoto wenye umri wa miaka 2 hadi 14, asilimia ya wazazi na walezi walioripoti kutumia viboko katika mwezi uliopita ilikuwa kuanzia 30% nchini Kazakhstan na 32% nchini Ukraine, hadi 63% nchini Serbia, 64% nchini Sierra Leone, na 77% nchini Togo.
Takwimu za kutisha barani Afrika
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO barani Afrika, viboko bado vimesalia juu zaidi duniani:
- Sierra Leone: Asilimia 64 ya watoto waliripoti kupigwa viboko majumbani katika mwezi uliopita.
- Togo: Asilimia 77 ya watoto walitandikwa viboko ikiwa moja ya viwango vya juu zaidi duniani.
- Mashuleni, takribani asilimia 70 ya watoto barani Afrika wanapitia viboko katika maisha yao ya shule, huku ripoti zikionesha kupigwa mara kwa mara, kuzabwa makofi na adhabu za kudhalilisha zikiwa za kawaida.
“Watoto barani Afrika wanalipia gharama ya mila zilizopitwa na wakati,” amesema Najat Maalla M’jid, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto akiongeza kuwa “Wakati nyumba na shule zote zinahalalisha vurugu, watoto hukua wakiamini kuwa ni jambo la kawaida. Tunapaswa kuvunja mzunguko huo.”
Shule pia si salama
Ripoti inaonesha kuwa viboko mashuleni pia vimesambaa sana. Barani Afrika na Amerika ya Kati, takribani watoto 7 kati ya 10 wanapitia adhabu ya viboko wakati wa masomo yao ya shule, ikilinganishwa na takribani robo tu katika eneo la Pasifiki ya Magharibi.
“Watoto hutumia muda mwingi nyumbani na shuleni. Wakati maeneo haya mawili yanahalalisha vurugu, yanaharibu usalama wao, utu wao, na imani yao kwa watu wazima,”amesisitiza M’jid.
Wito wa mageuzi ya kisheria na mabadiliko ya kiutamaduni
Licha ya miongo ya utetezi, ripoti imesema ni takribani nchi moja kati ya tatu pekee duniani zilizopiga marufuku kisheria adhabu ya viboko katika mazingira yote, ikiwemo nyumbani.
WHO inazitaka serikali kuimarisha ulinzi wa kisheria, kupanua kampeni za uhamasishaji, na kukuza mbinu mbadala za malezi zinazoheshimu haki za watoto.
“Hii ni zaidi ya kuvunja mzunguko wa vurugu,” amesema Dkt. Krug. “Tunapowalinda watoto dhidi ya adhabu ya viboko, tunawekeza katika familia zenye afya bora, jamii imara, na dunia yenye amani zaidi.”