Pedro Matos: Safari ya kutoka kuwa mhandisi wa masuala ya anga hadi mhudumu wa misaada ya kibinadamu
Pedro Matos: Safari ya kutoka kuwa mhandisi wa masuala ya anga hadi mhudumu wa misaada ya kibinadamu
Kabla ya Pedro Matos kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa miaka 17, kazi yake ya uhandisi wa masuala ya anga “haikutosheleza.” Mwanasayansi huyu kutoka nchini Ureno amekuwa akitumia ujuzi wake wa ramani na satelaiti kusaidia operesheni za kibinadamu, lakini sasa amekuwa mstari wa mbele kutoa msaada katika majanga, akivaa koti la WFP na buti.
Katika Siku ya Kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu , Bwana. Matos ameieleza UN News kuhusu historia yake.
Safari yake ya kuhudumu kwenye vimbunga hadi kwenye vita
Pedro amesema alitaka kuchukua ramani zake na kuwa yeye mwenyewe anayetoa msaada. Katika shirika la WFP, ameshughulika na operesheni za dharura na amesafiri kwenda nchi nyingi zilizo katikati ya migogoro, kama vile kimbunga Idai nchini Msumbiji na vita vya Ukraine.
Huduma za dharura ni kama kuendesha serikali
Kuratibu hatua za dharura ni sawa na “kuendesha serikali nzima”, ambapo kila shirika la Umoja wa Mataifa linachukuliwa kama “wizara”, na htua hizo hufanikiwa tu pale wote wanaposhirikiana katika maeneo manne ya msingi wakati wa majanga ambayo ni chakula, makazi, maji na afya.
Mara baada ya kurejea kutoka katika operesheni huko nchini Bangladesh, ameeleza jinsi walivyojitahidi kukabiliana na matatizo huko Cox's Bazar, kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani na makazi ya watu zaidi ya 700,000 waliokimbia vurugu kutoka Myanmar.
"Tumeweza kuwezesha mazingira bora zaidi kwa watu kuishi katika hali ya sintofahamu wakiwa na faraja kidogo ," amesema, huku akikumbuka pia ziara yake huko mwaka 2018 wakati mgogoro ulipokuwa mkubwa.
Wakati huo, "watu milioni moja walivuka mpaka ndani ya mwezi mmoja." Leo, ingawa bado hawajapata uhakika wa maisha yao ya baadaye, ameonesha maboresho kama vile nyumba na barabara zisizoharibika na mvua za masika, majiko ya gesi na kupanda miti upya."
Mafanikio na changamoto katika safari yake kama muhudumu wa misaada ya kibinadamu
Kazi hii imempatia mafanikio na bila kusahau changamoto.
Amesema matukio kama kutekwa nyara au kushambuliwa siyo katika yanayomkumba zaidi, bali ni matukio yanayowatokea wengine.
Hata hivyo, anakikumbuka kimbunga Idai kuwa ni miongoni mwa matukio magumu lakini yenye thawabu kubwa, kwani wameokoa maisha ya mamia ya maelfu ya watu.
Alipokuwa nchini Yemen, amesema, "tulishambuliwa kwa mabomu mara 20 kwa siku" katika mji mkuu, Sana'a. Ameongeza kuwa "kuna hali ya kawaida" isiyo ya kawaida ambayo hujengeka.
Amemeongeza kuwa"tunajikuta tukisema vitu kama, hapana, hilo halikuwa mbali sana, lilikuwa mita 500 tu kutoka hapa. Ni kitu ambacho kamwe sikuwahi kufikiri nitafikiri au kusema kabla ya kufanya kazi hii."
Alipofika katikati ya Ukraine wiki chache baada ya Urusi kuivamia, ameelezea hali hiyo kuwa "ngumu sana". Ndani ya wiki moja, yeye na wenzake walijikuta wakigawa pesa kwa watu waliokuwa wakitoka kwenye maeneo ya vita.
Kulisha mamilioni ya watu kila siku
Pedro ameelezea kuwa kiwango cha kazi ya kibinadamu ni kikubwa sana. “Sijawahi kufikiria kuwa nitakuwa ninalisha watu milioni 13 kwa siku huko Yemen,” amesema.
Ametoa wito kwamba kila taaluma inaweza kusaidia, kuanzia kwa wanasheria hadi wataalamu wa rasilimali watu, kwani kazi ya kibinadamu inafanana na kazi ya wazima moto au wafanyakazi wa kijamii.
Thamani ya Tuzo ya Nobel
WFP imetunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2020. Pedro amesema, “Kazi yetu haionekani sana, licha ya kulisha idadi ya watu milioni 120 kila siku.” Anaamini kwamba jukumu lake ni kuwapa sauti wale wasio na sauti. Somo muhimu zaidi ambalo amejifunza ni kwamba “Watu kimsingi ni wema."