Wewe pia unaweza kuwa mhisani - Hata msaada wa kalamu au tiba kwa watoto itatusaidia – Bi. Mwangi
Wewe pia unaweza kuwa mhisani - Hata msaada wa kalamu au tiba kwa watoto itatusaidia – Bi. Mwangi
Mary Anne Mwangi Katibu Mkuu wa shirika la kiraia la Priscilla and Angelica Chalks Foundation kilichoko kaunti ya Kajiado nchini Kenya anaelezea umuhimu wa uhisani akisema kupitia kazi ya usaidizi wa kiutu “tunaweza kusaidia na kubadilisha maisha ya watu wengi. Kama shirika letu tumeweza kusaidia watoto wengi ambao labda hawangeweza kupata masomo lakini kwa sasa wamepata masomo. Kuna wale ambao wameweza kusoma hadi Chuo Kikuu.
Bi. Mwangi alikuwa akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu kazi ya kituo chao ya kusaidia watoto wenye uhitaji wa kuanzia malazi, mavazi, chakula hadi elimu.
Haba na haba hujaza kibaba
Alipoulizwa kuhusu changamoto wanazokumbana nazo ametaja uhitaji mkubwa kuliko uwezo walio nao akisema, “unakuta mahitaji ni mengi kuliko kile ambacho mko nacho umepata. Uko mahali ambapo inahitajika kuchagua labda uko na watoto 100 na unahitaji kuchagua 10 hivyo unafanya kulingana na uwezo wako.”
Lakini vipi kuhusu mtazamo wa jamii kwa wahisani? Bi Mwangi anaanza na shukrani akisema, “ningependa kwanza kushukuru jamii yetu pale ambapo wamefanya na wanasaidia pale wanaweza. Hivyo si lazima uwe na uwezo mkubwa ili usaidie. Unaweza kuwa kitu kidogo, mfano kalamu. Unaweza kuwa na kitabu na uwezo wowote ule ambao unaweza Saidia.”
Afisa huyo akataja kile kinachohitajika zaidi kuwa ni elimu kwa watoto wanaowalea kwani anasema, “unakuta tu kuna watoto wengi sana hasa wale waliohitimu kidato cha 4 na hawezi kwenda Chuo kwa sababu hana fedha. Hilo ndilo eneo ambalo tukiweza kusaidia watoto wetu ili wanapomaliza shule hiyo hasa kidato cha 4 wanakuwa na stadi Na pia tuhakikishe na tusaidiane watoto wetu wote wamalize kidato cha 4.”
Mitandao ya kijamii yasaidia pia uwajibikaji
Kwa upande wa teknolojia amesema inawasaidia sana kwenye kazi zao. Sio tu kuonekana, bali pia wahisani kuthibitisha kile wanachofanya na fedha wanazopatia shirika hilo.
Uwajibikaji zaidi kupitia kile wanachochapisha kwenye mitandao ya kijamii na hata “mtu anaweza kuona maendeleo ya mtoto anayemgharimia elimu.”
Kwa Bi Mwangi faida kubwa ambayo ameipata ni msaada unaomwezesha kusaidia watoto wengine kusoma, na pia kupeleka mtoto hospitali na hata kuwapatia chakula, akitoa shukrani kwa shirika la Msalaba Mwekundu ambalo amesema linapatia wasichana taulo za kike.
Alipoulizwa nini kinampatia furaha, Bi. Mwangi akiwa na tabasamu usoni amesema “unaposomesha mtoto unaona yule mtoto ameweza kumaliza shule, ameweza kumaliza kweli, ameweza kupata kazi na kujisimamia kimaisha. Tunapata furaha sana kwa sababu tunaona ile athari chanya ya kile tunafanya. Unakuta mtoto kama yule naye anaweza kumsaidia mwingine na au hata hata asipomsaidia mwingine tayari maisha yake inatusaidia sana na inafurahisha na inatufanya tunaridhika sana.”
Watoto wanufaika wazungumza - "nimepata familia"
Miongoni mwa watoto wanufaika ni Jack Koech yeye anasema faida kuu ya kwanza ni elimu na ameweza kusoma elimu ya msingi hadi sekondari. Hivi sasasa anakaribia kuhitimu. Anashukuru kwa msaada aw mavazi na chakula.
Kwa Charline Kerubo, yeye kubwa ni kupata familia kwenye kituo hiki na ana matumaini ya kuhitimu hadi Chuo Kikuu na kupata kazi kwani waliohitimu hapo wamemtia na yeye moyo kuwa anaweza. Kwa sasa yuko kidato cha 3.