MONUSCO yalaani vikali mashambulizi ya ADF Beni na Lubero, DRC
MONUSCO yalaani vikali mashambulizi ya ADF Beni na Lubero, DRC
Umoja wa Mataifa kupitia Ujumbe wake wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (MONUSCO) umelaani vikali mashambulio ya hivi karibuni yaliyofanywa na Allied Democratic Forces (ADF) katika mikoa ya Beni na Lubero, Kaskazini mwa Kivu kati ya tarehe 9 na 16 ya mwezi huu wa Agosti.
Mashambulio haya yamesababisha vifo vya raia takribani 52 wakiwemo wanawake na watoto, imeeleza tarifa hiyo iliyotolewa leo Agosti 19 katika mji Mkuu wa DRC, Kinshasa.
Pia mashambulizi hayo yaliambatana na utekaji, uporaji na uharibifu wa mal iza wananchi.
Katika kushughulikia hali hii, MONUSCO imeongeza msaada wake kwa mamlaka za Kidemokrasia ya Congo ili kuboresha hatua za ulinzi wa raia.
“ADF, kikundi cha wapiganaji kinachojulikana kwa uhalifu wake katika eneo hilo, kimesababisha mlolongo wa matukio ya vurugu katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha wakazi maelfu kuhama na kuimarisha mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa DRC.” Imeeleza taarifa ya MONUSCO.
Makundi yarudi kwao
Aidha MONUSCO imesisitiza tena ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuyataka makundi yote kutoka nje ya nchi kuweka sulaha chini na kurejea katika nchi zao.
MONUSCO imeeleza kuwa inaendelea kujitolea kutekeleza jukumu lake la kulinda raia, kuunga mkono juhudi za serikali ya DRC za kurejesha utulivu, na kufanya kazi kuelekea amani ya kudumu katika eneo hilo.