Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu yafurutu ada UN yataka hatua za haraka zichukuliwe

Wafanyakazi wa UNRWA watoa msaada kwa familia iliyopoteza makazi yao katikati ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa huko Gaza.
© UNRWA Wafanyakazi wa UNRWA wanaendelea kuwaunga mkono raia wa Gaza.

Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu yafurutu ada UN yataka hatua za haraka zichukuliwe

Msaada wa Kibinadamu

Leo ni Siku ya Wahudumu wa Misaada ya Kibinadamu Duniani, na Umoja wa Mataifa unasema mwaka 2024 ulikuwa mbaya zaidi, kwani wahudumu 383 waliuawa duniani kote na mashambulizi mengi yalitokea Gaza na Sudan.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA imeonya leo katika Siku hii ya Wahudumu wa Kibinadamu Duniani kwamba takwimu hizo ni wito wa dharura wa kuwalinda raia na wale wanaohatarisha maisha yao kuwasaidia.

“Hata shambulio moja dhidi ya mhudumu wa misaada ni shambulio dhidi ya sisi sote na wale tunaowahudumia,” amesema Tom Fletcher, Msaaidizi wa Katibu Mkuu anayesimamia Misaada ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura.

Ameongeza kuwa “Mashambulizi haya kwa kiwango hiki, bila uwajibikaji wowote, ni shutuma ya aibu kwa kutokuchukua hatua na kutojali kwa jumuiya ya kimataifa.”

Wafanyakazi wa UNOPS waliovaa fulana za bluu wamesimama kwenye pampu ya mafuta katika Hospitali ya Ulaya huko Gaza.
UNOPS Wafanyakazi wa UNOPS watembelea hospitali huko Gaza.

Wahudumu wa kitaifa wako hatarini zaidi

Wengi wa waliouawa kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa walikuwa wahudumu wa kitaifa waliokuwa wakihudumia jamii zao, aidha walipokuwa wakitoa misaada au majumbani mwao. Mbali na waliouawa, 308 walijeruhiwa, 125 walitekwa nyara na 45 walikamatwa mwaka 2024 pekee.

Migogoro ya Gaza na Sudan ndiyo iliyokuwa hatari zaidi, umesema Umoja wa Mataifa ambapo watu 181 waliuawa  Gaza na 60 Sudan, na kusababisha ongezeko la asilimia 31 ya vifo ikilinganishwa na mwaka 2023.

Fletcher alisisitiza kuwa wahudumu wa kibinadamu “si shabaha ya mashambulizi, bali ni mnyororo wa uhai,” akizitaka serikali na wahusika wa kivita kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.

Vurugu zazidi kuongezeka mwaka 2025

Takwimu za mapema za Umoja wa Mataifa mwaka huu zinaonesha hali bado ni mbaya. Kati ya Januari na katikati ya Agosti 2025, tayari wahudumu 265 wa kibinadamu wameuawa, kwa mujibu wa hifadhi takwimu za Usalama wa wahudumu wa misaada.

OCHA imesema mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada yaliongezeka katika nchi 21 mwaka 2024, huku wtendaji wa serikali wakitajwa mara nyingi zaidi kama wahusika wakuu.

“Haya si makosa ya vita,” Fletcher alisema. “Ni maamuzi yaliyofanywa kwa kupuuza sheria na ubinadamu wenyewe.”

Sheria za kimataifa zimepuuzwa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 2730 mnamo Mei 2024, likiwataka wahusika wote wa mizozo kuwalinda wahudumu wa misaada na kudai uchunguzi huru wa ukiukaji. Hata hivyo, ukosefu wa uwajibikaji bado unaendelea.

“Vurugu dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu si jambo la lazima.Ni  lazima likome,” Fletcher amesisitiza, akitaka wahalifu wafikishwe mbele ya sheria.

Mfanyakazi UNICEF aliyevaa kitambaa cha bluu kichwani na gauni jeusi, akiwa na kitambaa cha mkono UNICEF , anachunguza mkono wa mtoto huku bibi yake mtoto akimtazama. Kikombe cha waridi kimewekwa sakafuni karibu.
© UNICEF/Arezo Haidary Mhudumu wa afya akitembelea familia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Katibu Mkuu: Shambulio dhidi ya wahudumu wa kibinadamu ni shambulio dhidi ya ubinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake maalum wa siku hii ameungana na wito wa kuchukua hatua za dharura, akisisitiza kwamba wahudumu wa kibinadamu ndio mnyororo wa mwisho wa uhai kwa zaidi ya watu milioni 300 waliokwama katika migogoro na majanga.

“Sheria za kimataifa ziko bayana wahudumu wa misaada lazima waheshimiwe na kulindwa. Hawawezi kamwe kulengwa,” amesema Guterres. Na kuongeza kuwa “Lakini mipaka inavukwa bila adhabu. Kinachokosekana ni ari ya kisiasa na ujasiri wa kimaadili.”

Kuwaenzi waliopoteza waisha wakitoa huduma

Katika kuadhimisha siku hii, Umoja wa Mataifa umerejesha kampeni yake ya kimataifa ya #ActForHumanity, ukizitaka serikali, jamii na watu binafsi kusshikamana na wahudumu wa misaada. Katibu Mkuu ametaka kuwe na uwekezaji katika usalama wao, uwajibikaji thabiti zaidi, na kusitishwa kwa uuzaji wa silaha kwa makundi yanayokiuka sheria za kimataifa.

Amehitimisha ujumbe wake akisistiza “Pamoja, tuseme kwa sauti moja shambulio dhidi ya wahudumu wa misaada ni shambulio dhidi ya ubinadamu”.

Volker Türk, afisa UN , anaonekana akizungumza na kundi la watu nje nchini Sri Lanka.
© OHCHR/Anthony Headley Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu Volker Türk akiwa na familia za wakimbizi wa ndani Trincomalee, Sri Lanka

Kamwe hatutosahau mchango muhimu wa wahudumu wa kibinadamu: Türk

Huko Geneva Katika hafla maalum ya kuadhimisha siku hii, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amewakumbuka waliopoteza maisha, wakiwemo wahudumu 22 waliouawa Baghdad mwaka 2003, na kuongeza“Kamwe hatutaacha kusisitiza kwamba serikali au nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wafanye kazi pamoja kuhakikisha wanatoa fursa ya ufikiaji wa kibinadamu kwa watuwenye uhitaji na kunakuwepo na uwajibikaji wa ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu zikijumuisha ulinzi kwa wahudumu wa kibinadamu na wa Umoja wa Mataifa”.

Ameongeza kuwa katika siku hii ya Wahudumu wa Kibinadamu Duniani, nawaenzi wahudumu wa misaada waliopoteza maisha yao wakihudumia wengine, huku heshima maalumu nikiilelekza kwa wafanyakazi wenzangu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi kwa bidii duniani kote.

Amesema “Licha ya kukabiliana na hatari kubwa, wanaendelea kulinda na kusaidia jamii zilizo hatarini, wakionyesha ujasiri na kujitolea. Uaminifu wao thabiti hauokoi tu maisha bali pia unaimarisha azma ya pamoja ya kutetea utu wa binadamu na kuendeleza thamani za kibinadamu kila mahali.”