Gaza, tishio lililo kimya
Gaza, tishio lililo kimya
Umoja wa Mataifa umetenga siku maalum ya kuwashukuru watoa huduma za misaada ya kibinadamu na siku hiyo ni Agosti 19 kila mwaka. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu zinaeleza kuwa mwaka huu wa 2025, watu milioni 305.1 kutoka nchi 72 wanahitaji usaidizi wa kibinadamu ambao utagharibu dola bilioni 47.4. Takwimu hizi zinaonesha umuhimu na uhitaji wa watoa huduma wa kibinadamu.
Katika kuadhimisha siku hiyo mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yameandaa vitu mbalimbali kuwashukuru wahudumu hawa wa kibinadamu kwa ushujaa wao na miongoni mwa mashirika hayo ni lile la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Watoto UNICEF ambalo lenyewe limetengeneza Makala maalum ikiwaangazia watumishi wawili ambao walifanikisha utoaji chanjo ya polio kwa Watoto karibu 600,000 katikati ya vita huko Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel.
James Elder ni msemaji wa UNICEF anaeleza zaidi kuhusu makala hiyo iliyopewa jina Gaza, tishio lililo kimya “GAZA, TISHIO LILILO KIMYA ni ushuhuda wenye nguvu wa ustahimilivu wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu katika kukabiliana na hatari zilizo kwenye migogoro. Makala hii ya nusu saa imewafuatia Dkt. Younis Awadallah na Fairuz Abuwarda, ambao katikati ya sitisho la muda mfupi la vita kwa sababu za kibinadamu mwaka jana, waliwasilisha chanjo za kuokoa maisha kwa watoto kote Ukanda wa Gaza. Ujasiri wao unatoa msisitizo muhimu wa kuwa, pale kanuni muhimu za kibinadamu zinapoheshimiwa, ndio hapo watoa huduma za kibinadamu wanapopewa usalama wa kuingia kwenye eneo la mizozo, na maisha ya watoto yanaokolewa.”
Unaweza kutazama video hiyo kwa kubofya hapa
Video ya UNICEF imemuonesha mtaalamu wa afya Dkt. Younis Awadallah, huyo ni Daktari mstaafu na Mfanyakazi wa zamani wa UNICEF huko Palestina akitembea katika mabaki ya nyumba zilizoshambuliwa na makombora na Israel kuwafuata watoto kila waliko ili kuwapatia chanjo ya polio.
Dkt akiwa na matumaini anaeleza kuwa “Kupitia kampeni hii ya chanjo, tumejaribu kufikia kila mtoto. Tumeweza kutoa chanjo kwa karibu watoto 600,000 katika wakati mgumu sana, katikati ya vita. Kwa kweli ninatumaini jitihada zaidi zinafanywa ili kuwasaidia watoto hawa walio hatarini, kuwalinda na magonjwa, kuhakikisha kwamba wanapata maji safi ya kunywa, kutibu magonjwa hatari, na kuwaandalia chakula cha kutosha ili kuzuia utapiamlo.”
Chakusikitisha ni kuwa pamoja na juhudi kubwa za watoa huduma kama Dkt Younis Awadallah, lakini hali ya watoto huko Gaza ni mbaya sana, watoto wanakufa kwa njaa, utapiamlo unazidi kuchukua maisha yao, maji hakuna, chakula hakitoshi na mabomu yanazidi kuchukua uhai wa wengi kila siku.
Makala ya UNICEF ya Gaza, tishio lililo kimya inatupa changamoto kwa kila mtu kutambua kwamba kulinda maisha ya binadamu sio tu wajibu wa kisheria chini ya sheria za kimataifa, bali ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata haki ya kuishi huko Gaza na katika mazingira mengine ya mizozo.