Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mhudumu wa kibinadamu arejea nyumbani Sudan kutoka ukimbizini Uganda

Naibu Katibu Mkuu wa UN katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura Tom Fletcher (Katikati) akiwa katika kambi moja ya waliohamishwa huko El Genina, Darfur.
OCHA Naibu Katibu Mkuu wa UN katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura Tom Fletcher (Katikati) akiwa katika kambi moja ya waliohamishwa huko El Genina, Darfur.

Mhudumu wa kibinadamu arejea nyumbani Sudan kutoka ukimbizini Uganda

Msaada wa Kibinadamu

Adam Ibrahim alikuwa akifanya kazi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) nchini mwake Sudan wakati vita vilipozuka.

Alilazimika kukimbia pamoja na familia yake, lakini alirudi kusaidia watu waliokuwa wameathirika vibaya na vita jimboni Darfur. Huu hapa ni ushuhuda wake.

Nilikuwa nyumbani nikimsaidia binti yangu kujisomea kwa ajili ya mtihani wa darasa la sita uliopangwa kufanyika siku iliyofuata. Kisha, ghafla, milio mizito ya risasi ilivunja utulivu katika mji wangu wa Zalingei, makao makuu ya Jimbo la Darfur ya Kati,” amesema Adam Ibrahim.

Picha ya anga kutoka google ya Zalingei mnamo tarehe 8 April 2023.
© Google Earth Picha ya anga kutoka google ya Zalingei mnamo tarehe 8 April 2023.

Zalingei bado inakumbwa na hali ya ukosefu wa usalama na uhaba mkubwa wa huduma za msingi.

Ameendelea kusema, mwanzoni alifikiri milio hiyo ingepita haraka. Akakimbilia kununua chakula na maji ya kutosha kwa siku sita. Lakini mtaa ikageuka kuwa uwanja wa mapambano. Kitu pekee amekiweza kufanya ni kujaribu kulinda familia yake.
Licha ya hali hiyo ya vurugu, ameendelea kufanya kazi.

“Umeme na intaneti vilikuwa vinakatika mara kwa mara, lakini nilihakikisha simu yangu imejaa chaji ili kutuma taarifa za kila siku kwa Mkuu wa Ofisi wa OCHA. Hilo lilinipa sababu ya kuendelea hata katika hali ya sintofahamu,”ameongezea.

Hatimaye hali ikawa hatari mno kubakia nyumbani

Juni 2023: Safari ya ukimbizi

Baada ya siku 39 za sintofahamu, familia ya watu 10 ya Adam ilianza safari ya kuikimbia Sudan. Walipitia Nyala, Kosti, hadi kuvuka mpaka kuingia Sudan Kusini na baadaye Uganda nchi ambayo alikuwa amesikia kuwa na utulivu na mfumo mzuri wa elimu kwa watoto. Safari kwa gari ilichukua siku 23. Watoto hawakuwa na hati ya kusafiria, na wakati huo hakukuwa na kambi za wakimbizi kwa raia wa Sudan.

Adam akiwa na binti zake wawili nchini Uganda.
© UNOCHA/Adam Ibrahim Adam akiwa na binti zake wawili nchini Uganda.

Kwa furaha yangu, maafisa wa uhamiaji katika nchi zote mbili walikuwa wema na wa msaada. Tulipofika Kampala, ndani ya siku tatu tulikodi nyumba na tulipewa hadhi ya hifadhi ya ukimbizi. Niliposhika kadi zetu za ukimbizi mikononi mwangu, nilivuta pumzi kwa kina na kusema, “Tumefika salama.” Niliandikisha watoto wangu shuleni na nikaanza kufanya kazi mtandaoni, hatimaye nikapata hali fulani ya utulivu.”anasema.

Huko Uganda, maisha yalianza kuwa na mwelekeo mpya. Lakini ndani yake, hamu ya kurudi kusaidia watu wa taifa lake haikufa.

Novemba 2024: Kurudi Zalingei- Uamuzi mgumu, lakini wa maana

Miezi kadhaa baadaye, Adam alifanya uamuzi mgumu wa kurudi Sudan – akiiaacha familia yake salama Uganda. “Nilirudi Zalingei nikiwa na moyo mpya wa kuwahudumia wale waliobaki kwenye mateso yale yale ambayo nilikuwa nimeyakimbia, pia nilikuwa mtoa riziki pekee wa familia yangu, na ilinibidi kuhakikisha wanaweza kuishi Uganda,” anasema.

Wasudan wanaowasili wakishusha mizigo yao kutoka kwa lori katika kituo cha mapokezi kaskazini magharibi mwa Uganda.
© UNHCR/Ssozi Mukasa Daniel Wasudan wanaowasili wakishusha mizigo yao kutoka kwa lori katika kituo cha mapokezi kaskazini magharibi mwa Uganda.

Mji wangu wa nyumbani umebadilika

Zalingei aliyoirudia haikuwa ile aliyoikimbia, hakuitambua tena. Nyumba yake ilikuwa imeporwa, imeharibiwa na imekaliwa na familia nyingine – daktari na familia yake waliokuwa wamepoteza makazi yao.

Adam aliwakaribisha kwa moyo mkunjufu, akitenga sehemu ndogo ya nyumba kwa ajili yake na mfanyakazi mwenzake.

Nyumba ilikuwa imelengwa na uporaji; madirisha yalikuwa hayapo na mali zetu zilikuwa zimepotea. Nilitarajia kupata vyeti vya shule vya watoto wangu, picha, au hati nyingine yoyote tuliyoiacha. Lakini vyote vilikuwa vimepotea,” amesema.

Anaongezea kuwa “Kila mtu alikuwa na silaha, hata watoto wa umri wa miaka 15. Watu walikuwa na hofu, wameshikwa na mshtuko, na kila mara wakijiandaa kwa ghasia nyingine.”

Safari hadi El Geneina

Alihitajika El Geneina, Darfur Magharibi – mji uliokuwa umeathirika zaidi na ghasia – na watu wake walihitaji msaada wa kibinadamu kwa haraka.

Mitaa ilikuwa imejaa magari ya kijeshi yaliyoteketezwa. Makundi yaliyojihami na  silaha wakilinda mitaa kwa magari yaliyo na bunduki nzito juu yake,” amesema.

Ramani ya Google Earth ya Zalingii kuanzia tarehe 21 Machi 2025 ikiwa na dalili zinazoonekana za uharibifu wa nyumba katika sehemu ya kusini ya jiji.
© Google Earth Ramani ya Google Earth ya Zalingii kuanzia tarehe 21 Machi 2025 ikiwa na dalili zinazoonekana za uharibifu wa nyumba katika sehemu ya kusini ya jiji.

Mahitaji ya kibinadamu yalikuwa makubwa chakula, maji, huduma za afya na makazi yalihitajika, lakini misaada ilikuwa finyu.

Licha ya changamoto, waliweza kutoa msaada.  “Hata hivyo, tulifanya yote tuwezayo. Kati ya mwaka 2023 hadi 2025, tuliwafikia zaidi ya watu 800,000 waliopoteza makazi katika Darfur Magharibi na Kati, kwa msaada muhimu.”

Pia alishirikiana na  OCHA nchini Chad kuratibu misafara ya misaada kuvuka mpaka kuingia Darfur. Misafara hiyo ilikuwa njia pekee ya kupeleka chakula, dawa, na vifaa kwa jamii zilizokuwa zimekatwa na vita.

Familia, kujitolea na matumaini kwa Sudan

Leo hii, Adam yupo tena Sudan. Familia yake bado iko Uganda, na huwa anawatembelea mara moja kwa mwaka lakini kutengana nao kunaumiza.

Sudan ni moja ya migogoro mikubwa na changamano zaidi ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni 30.4 – zaidi ya nusu ya idadi ya watu – wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa dharura, lakini Ombi la usaidizi kwa Sudan kwa mwaka 2025 limefadhiliwa kwa asilimia 13.3 pekee hadi sasa.