Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya Mwl. Nyerere ya uandishi bunifu kuvutia utamaduni wa kuandika nchini Tanzania

Esther Karin Mngodo, Mjumbe wa kamati inayoratibu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu nchini Tanzania.
UNNews
Esther Karin Mngodo, Mjumbe wa kamati inayoratibu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu nchini Tanzania.

Tuzo ya Mwl. Nyerere ya uandishi bunifu kuvutia utamaduni wa kuandika nchini Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Baada ya Umoja wa Mataifa kutenga siku maalum ya kuadhimisha siku ya lugha ya kiswahili duniani ambayo hufanyika Julai saba kila mwaka, nchi mbalimbali zimekuwa zikiwahamasisha wananchi wake kuchangamkia fursa ziletwazo la lugha ya Kiswahili. Taasisi ya Elimu ya nchini Tanzania- TET iliyo chini ya wizara ya Elimu yenyewe imeenda mbali zaidi na inatoa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Akihojiwa jijini New York Marekani na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa mjumbe wa kamati inayoratibu tuzo hizo Esther Karin Mngodo ameeleza kuwa ulimwenguni kote watu wanapambana kukuza lugha zao na ndio maana wameamua kuja na tuzo za uandishi bunifu wakitaka kuonesha umuhimu wa waandishi.

“Tuzo hii imeanzishwa kwa lengo la kuwatunuku waandishi mahiri. Sote tunajua kwenye jamii tunao waandishi, lakini wengine hawajapewa nafasi ya kutambulika na jamii, lakini pia ni fursa nzuri ya kukuza lugha ya Kiswahili. Najua lugha yoyote ambayo haina maandishi haiwezi kupewa kipaumbele.’

Tuzo hizo zinafunguliwa rasmi tarehe 15 Agosti na kufungwa tarehe 30 Novemba 2025 na zitatolewa mwezi April 2026.

Ameeleza kuwa katika jamii wamekuwa wakiona watu wakisoma vitabu hususan kwa lugha zingine za kigeni ndio maana na wao wanaendesha tuzo hizo ili kupata watu wakuandika vitabu na kukuza sekta ya uchapishaji wa vitabu. “Ndio maana wale washindi nafas iza kwanza basi kitabu chake kinachapishwa kwa gharama za serikali “

Tuzo hii inalenga kuonesha kwamba Kiswahili sio tu lugha ya mtaani, yaani lugha ambayo haiheshimiki bali ni lugha ya kirafiki na ina watu wao ambao ndio sisi wenyewe na tunao waandishi, na waandishi hao sio watu baki ni watu wanaopewa heshima ndio maana ngazi ya kitaifa yani serikali ikaona ni muhimu sana kuwatunuku waandishi.

Washiriki

Mngodo ameeleza ni watu aina gani ambaye anaweza kushiriki katika tuzo hizo

“Watu wa aina mbalimbali wanaruhisiwa kuwania tuzo hizo, iwe ni mfanyakazi wa ndani, askari polisi, waalimu, wanafunzi. Mtu wa umri wowote, ili mradi tu awe ni Mtanzania na anaandika kwa lugha ya Kiswahili anaruhusiwa kuleta kazi yake.

Vipengele vinavyo waniwa

Bi. Mngodo ameeleza hapo awali tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu , ilipoanza kulikuwa na maeneo mawili ya kushindaniwa ambayo ni ushairi na  riwaya na sasa wameongeza na kufikia nne.

“Maeneo ambayo tumeongeza ni hadithi za watoto na tamthilia. Kwahiyo kila nyanja ina vigezo vyake mahususi ambayo imebeba. Niwaombe washiriki wanaotaka kushiriki wafuatilie katika mitandao ya kijamii Instagram, X (Twitter), Facebook accont yetu inaitwa @tuzonyerere huko kote watapata kujua vigezo  mahususi vya kila nyanja.

Esther Karin Mngodo (kulia), Mjumbe wa kamati inayoratibu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu nchini Tanzania akiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.
UN News
Esther Karin Mngodo (kulia), Mjumbe wa kamati inayoratibu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu nchini Tanzania akiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Mshindi anapata nini?

Washindi kumi wanatambulika kwa kupewa cheti, lakini washindi watatu bora wanapewa zawadi ya fedha taslimu ambapo mshindi wa tatu anapewa milioni tano, (sawa na takriban dola 2000) mshindi wa pili milioni saba ( sawa na takriban dola 2800) na mshindi wa kwanza anapewa shilingi milioni kumi za Kitanzania (sawa na takriban dola 4000) na kazi yake inachapishwa kwa gharama za serikali na kusambazwa kwenye maktaba na shule.

Mjumbe huyu wa kamati ya tuzo amewashauro wale wote wenye nia ya kushiriki kuwasilisha kazi zao mapema. “Kusubiri mpaka dakika ya mwisho alafu unaanza kutafuta  koma iko wapi na nukta iko wapi sio sawa. Unaweza kuleta mswada ambao haujawekwa vizuri, ukisikia dirisha limefunguliwa basi karibu ulete kazi yako na bila shaka unaweza kuwa mshindi wa milioni kumi.

Akihitimisha mahojiano haya amewashauri wale ambao wanasema hawapendi kuandika kwani ni kitu kigumu kufanya mazoezi kwani tayari watu wengi wanaandikiana kwenye mitandao ya kijanii akitolea mfano WhatsApp.

Licha ya Umoja wa Mataifa kutangaza tarehe saba Julai kuwa siku ya Kimataifa ya lugha ya kiswahili duniani bado baadhi ya watu hawachukulii hiyo kama fursa kwani na kwa hao amewaasa kuwa “Kiswahili kinakua, lazima tukiri tukumbatie lugha yetu na tuipende lugha yetu… Nadhani miaka michache ijayo utashangaa sana kwani itaendelea na kuwa sio tu lugha ya Afrika, lakini itafika sehemu kuwa lugha ya dunia nzima.