Manusura wa ukatili wa kingono wahitaji msaada wa kivitendo si ahadi – Ripoti
Manusura wa ukatili wa kingono wahitaji msaada wa kivitendo si ahadi – Ripoti
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imebaini ongezeko kubwa la visa vya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, na kutoa wito wa kuimarishwa kwa huduma za kusaidia manusura.
Kwa mujibu wa Ripoti hiyo ya 16 ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye maeneo yenye mizozo iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, zaidi ya manusura 4,600 waliripotiwa kufanyiwa ukatili huo mwaka 2024 — ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
ikiwa ina kurasa 34, ripoti hiyo inahusisha nchi 21 ambazo taarifa zake zimethibitishwa na Umoja wa Mataifa na inaonesha kuwa ukatili ulifanywa na vikundi vya kiserikali na visivyo vya kiserikali, kama mbinu ya vita, mateso, ugaidi na ukandamizaji wa kisiasa.
DRC, Sudan Kusini, Somalia na Haiti zaongoza
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Haiti, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Somalia na Sudan Kusini zinaongoza kwa kuwa na matukio mengi zaidi ya ukatili wa kingono kwenye maeneo yenye mizozo.
Waliokumbwa na visa hivyo ni pamoja na wanawake, wasichana, wanaume, wavulana, pamoja na watu wa mwelekeo tofauti wa kijinsia, jamii za wachache na watu wenye ulemavu.
Umri wa manusura ni kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 75, na ripoti inasema, “asilimia 92 ya manusura wote 4,600 ni wanawake.”
Ripoti pia inafichua kuwa ukatili wa kingono ulienea kwenye maeneo watu wanakoshikiliwa kizuizini, ukifanywa kama njia ya mateso, udhalilishaji na kupata taarifa.
Vikundi vya waasi vilitumia ukatili huo kama njia ya kutawala maeneo, rasilimali na kuendeleza itikadi kali. Pia, upatikanaji mkubwa wa silaha ndogo ndogo uliendelea kuchochea vitendo hivi.
Kauli ya Bi. Patten
Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye mizozo, amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema kuwa ukosefu wa upatikanaji wa huduma za afya na msaada wa kisaikolojia unawaacha manusura wengi kwenye hatari kubwa, hasa ndani ya saa 72 za baada ya kukumbwa na ukatili ambapo matibabu ya haraka ya ukatili wa kingono huhitajika zaidi.
Nini kifanyike?
Ripoti inashauri kuongeza ufadhili kupitia Mfuko wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Ukatili wa Kingono kwenye mizozo, pamoja na kutumwa kwa washauri wa ulinzi wa wanawake katika maeneo ya migogoro.
Ripoti ina kiambatanisho kilichotaja kwa mara ya kwanza jumla ya pande 63 za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazohusishwa na mifumo ya ubakaji na ukatili mwingine wa kingono, kutokana na ushahidi uliothibitishwa na Umoja wa Mataifa.
Baadhi yao, Hamas wa eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, RED Tabara nchini DRC, na mashirika kadhaa ya usalama nchini Libya.
Ripoti kwa mara ya kwanza pia imeweka "orodha ya tahadhari", ikielekeza lawama kwa vikosi vya Israeli na Urusi kwa madai ya ukatili wa kingono kwenye maeneo ya korokoroni, huku ikieleza kuwa kukosekana kwa upatikanaji wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa kunakwamisha uthibitishaji wa kina.
Wito wa Guterres
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ametoa wito kwa pande zote katika migogoro kuhakikisha kuwa hatua madhubuti za kuzuia ukatili wa kingono zinawekwa, ikiwa ni pamoja na kutoa maagizo wazi ya kupiga marufuku ukiukaji huo, kuwawajibisha wahusika na kuruhusu Umoja wa Mataifa kutoa huduma muhimu.
Na kwa Patten, "hatupaswi kuwapa manusura maneno ya matumaini pekee, bali maisha ya utu na hatua thabiti za kukomesha uhalifu huu.”