WFP yasitisha kwa muda safari za anga Solle, Burkina Faso
WFP yasitisha kwa muda safari za anga Solle, Burkina Faso
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesitisha kwa muda safari za anga za kupeleka misaada ya kibinadamu huko Solle, kaskazini-magharibi mwa Burkina Faso kufuatia ajali ya Jumatatu.
Mlipuko uisikika punde baada ya helikopta kutua na mtumishi mmoja wa ndege na mmoja wa serikali walijeruhiwa wanaendelea na matibabu na WFP inachunguza tukio hilo.
Helikopta imepata uharibifu mdogo lakini imehamishwa kwa usalama kutoka Solle.
Taarifa ya WFP iliyotolewa Dakar, mji mkuu wa Senegal, inasema shughuli za anga za WFP ni muhimu sana kwa kupeleka misaada muhimu kwa jamii zilizo ngumu kufikiwa na zenye uhitaji mkubwa nchini Burkina Faso.
Katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro huko Burkina Faso, WFP imepanga kuwafikia idadi ya watu 315,000 walio hatarini zaidi katika msimu wa mwambo ambao ni kuanzia mwezi Juni hadi huu wa Agoti, wakati akiba ya chakula ya familia imeisha.
WFP inathibitisha tena dhamira yake isiyoyumba ya kusaidia jamii zenye uhitaji na kufika katika maeneo ya mbali zaidi na misaada ya kibinadamu.