Chonde chonde turuhusuni tufikie wahitaji El Fasher, Sudan – WFP
Chonde chonde turuhusuni tufikie wahitaji El Fasher, Sudan – WFP
Njaa imetulazimisha kukimbia nyumbani hadi kufika hapa kwenye kambi ya wakimbizi ya Tawila,” amesema mtoto wa kike mwenye umri wa miaka huko Sudan ambako mapigano kati ya jeshi la serikali, SAF na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka, RSF yaliyoanza Aprili 2023 yamefurusha mamia ya maelfu ya watu.
Mtoto huyo aitwaye Sondos amesema hayo kupitia makala iliyochapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwenye wavuti wake Agosti 13 2025.
Akiwa Tawila ambako ni kilometa 75 kutoka El Fasher walikokimbia, Sondos ambaye na familia yake wameishi kwa wiki kadhaa kwa kula mtama pekee anasema, "Ni njaa tu na mabomu. Makombora yalikuwa yanamiminika kama mvua kwenye mji wa El Fasher.”
Kwa familia za wakimbizi wa Tawila, njaa na migogoro ni mambo yanayohusiana kwa karibu. Mama mmoja, Jamila, ameeleza jinsi dada yake alivyofariki kwa njaa mapema mwaka huu katika kambi ya Zamzam.
“Jambo mbaya zaidi tulilokumbana nalo ni njaa na kupoteza ndugu zetu. Ni vigumu kumpoteza ndugu milele. Njaa inayodumu hadi leo ni ngumu sana.” anasema.
Leo hii, mamia ya maelfu ya watu bado wamekwama katika jiji la El Fasher na wanakabiliwa na njaa kali, kwani mji huo haupati msaada wa kibinadamu ikiwemo chakula kutoka WFP.
Eric Perdison, Mkurugenzi wa WFP kwa ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika amesema, “Kila mtu El Fasher anakabiliana na mapambano ya kila siku ya kuishi. Njia zote za kujikimu zimeisha kutokana na vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili.”
Raia El Fasher wanaishi kwa kula majani
WFP inataka ruhusa ili iweze kufikisha mahitaji kwa raia huko El Fasher ambako kikosi cha RSF kimeuzingira tangu mwaka jana.
Huko El Fasher, baadhi ya wakazi wanasemekana kuishi kwa kula majani ya mifugo na mabaki ya chakula. Ingawa WFP inaendelea kutoa msaada wa pesa za kidijitali kwa takriban watu robo milioni katika mji huo, ili waweze kununua chakula kinachopatikana sokoni, msaada huo ni mdogo sana ikilinganishwa na mahitaji yanayoendelea kuongezeka – na hivyo kuhitajika kwa dharura misaada ya chakula ya moja kwa moja kwa kiwango kikubwa.
Kama Sondos na familia yake, wengi walioweza kuondoka El Fasher wamekimbilia Tawila. Lakini mahema ya muda jangwani hayatoi ulinzi wowote dhidi ya msimu wa mvua unaoanza sasa.
Malori ya chakula yako tayari kusafiri
Corinne Fleischer, Mkurugenzi wa Ugavi na Usambazaji wa WFP anasema, “WFP iko tayari na malori yaliyojaa msaada wa chakula kuingia El Fasher. Tunahitaji kwa dharura dhamana ya kupita salama.”
WFP imepokea idhini kutoka Tume ya Misaada ya Kibinadamu ya Port Sudan kwa msafara wa misaada kupelekwa El Fasher. Lakini RSF, ambao wamelizingira jiji hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja, bado hakijatoa tamko la kuunga mkono kusitisha mapigano ili kuruhusu bidhaa za kibinadamu kuingia.
Vita Sudan vimesababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani, ambapo watu milioni 25, ambayo ni nusu ya idadi ya watu wote nchini Sudan, wanakabiliwa na njaa kali, na wanawake na watoto milioni 3.5 wanakabiliwa na utapiamlo.