Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama tembezi yaleta haki na amani Greater Pibor, Sudan Kusini

Baadhi ya watu, wakiwemo makamishna, viongozi wa jumuiya, vijana, na wawakilishi wanawake hivi karibuni walishiriki katika kongamano la amanilililoandaliwa na UNMISS Sudan Kusini.
UNMISS/Denis Louro
Baadhi ya watu, wakiwemo makamishna, viongozi wa jumuiya, vijana, na wawakilishi wanawake hivi karibuni walishiriki katika kongamano la amanilililoandaliwa na UNMISS Sudan Kusini.

Mahakama tembezi yaleta haki na amani Greater Pibor, Sudan Kusini

Amani na Usalama

Mahakama tembezi iliyopelekwa katika eneo la utawala la Greater Pibor, Kaunti ya Pibor jimboni Jonglei Mashariki mwa Sudan Kusini imeleta haki na amani kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo.

Greater Pibor imebarikiwa na tamaduni na historia iliyochangamka Jamii zake husherehekea utambulisho wao kupitia mavazi ya kitamaduni, sherehe, na desturi za kiroho zinazowaunganisha. 

Hata hivyo, wizi wa mifugo, unaoambatana na ukatili wa kingono na utekaji wa watoto ni mambo ambayo pia yamekita mizizi katika tamaduni na kuwa chanzo kikuu cha migogoro kati ya jamii.

Mara nyingi, wahalifu wa uhalifu kama huu hawaadhibiwi. Hata hivyo, mahakama mpya ya kuhamahama, iliyopelekwa katika Kaunti ya Pibor kwa msaada wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) na Mfuko wa Upatanisho, Mnepo na Usalama wa Sudan Kusini, inasaidia kupambana na hali hii ya kihistoria ya wahalifu kutoadhibiwa.

Geetha Pious, Mkuu wa Ofisi ya UNMISS katika eneo hilo anasema, “Kuna ongezeko la watu kuamini mfumo wa haki, watu kuwasilisha kesi zao kwenye vyombo vya haki. Hii ni mafanikio makubwa kwa idara nzima ya mahakama, majaji, mawakili, na naamini hii ndiyo njia ya kusonga mbele. Tunapaswa kuendeleza kasi hiyo kwa sababu mahakama na mfumo wa haki ni muhimu na ni wa msingi kwa amani na maendeleo endelevu ya jamii yoyote.”

UNMISS ina takwimu kwamba kwa kipindi cha wiki nne, mahakama hiyo imesikiliza kesi 16 ngumu za jinai na kufanikisha hukumu za kifungo kwa wahalifu watano. Kesi nyingine 10 za kiraia, nyingi zikihusu migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi ni chanzo kikuu cha mvutano na migogoro, pia zimeamuliwa.

Sebit Bullen Lako, ni Jaji wa Mahakama Kuu nchini Sudan Kusini anasema, “Mtu wa mwisho hapa, alimuua mtu, kisha wakaenda polisi, wakaripoti suala hilo na kumpeleka mtuhumiwa mahakamani. UNMISS, kupitia mpango wa kusaidia mahakama ya kuhamahama, imewasaidia sana watu wa Sudan Kusini, imeokoa maisha ya wengi kwa sababu, kizazi kama hiki cha hapa Pibor, wanapochukua sheria mkononi vifo vinaweza kuongezeka, kwa kuwa wanaweza kutumia bunduki moja kwa moja.”