Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN WOMEN: Afghanistan bado ina pengo kubwa la kijinsia

 Ndoa za utotoni ni mkakati wa maisha kiuchumi nchini Afghanistan huku familia zikiwaoza binti zao ili kupunguza mzigo wao wa kiuchumi.
© UNICEF/Madhok
Ndoa za utotoni ni mkakati wa maisha kiuchumi nchini Afghanistan huku familia zikiwaoza binti zao ili kupunguza mzigo wao wa kiuchumi.

UN WOMEN: Afghanistan bado ina pengo kubwa la kijinsia

Wanawake

Ikiwa ni miaka minne tangu Taliban kuchukuwa madaraka, wanawake na wasichana wa Afghanistan wanaendelea kukabiliwa na vizuizi vya kisheria na kijamii vinavyowazuia kushiriki katika maisha ya umma, limesema shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN WOMEN.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa UN Women kutoka Kabul Afghanistan na New York Marekani imeeleza kuwa hakuna hata amri moja kati ya zilizowekwa tangu mwaka 2021 iliyobatilishwa, hali inayoongeza hatari ya “kuhalalishwa” kwa mgogoro mkubwa zaidi wa haki za wanawake duniani.

Wasichana wamezuiwa kuhudhuria shule baada ya kufika umri wa miaka 13, wanawake wamepigwa marufuku kushiriki katika ajira nyingi, siasa, na katika baadhi ya maeneo hata kutembea mitaani bila kuandamana na wanaume.

Wanawake na wasichana pia wanakabiliana na vikwazo vya kusomea masuala ya tiba na marufuku ya kutibiwa na madaktari wanaume, na hivi vimeongeza changamoto za kupata huduma za afya, huku misaada ya kigeni ikipungua.

Makatazo yote haya matokeo yake ni ongezeko la vifo vya akina mama wajawazito, ndoa za utotoni, na ukatili dhidi ya wanawake. Afghanistan sasa inashikilia nafasi ya pili duniani kwa pengo kubwa la kijinsia.

Hata hivyo, UN Women imeeleza bado kuna matumaini kwani wanawake wa Afghanistan wanaendelea kuonesha ujasiri na ustahimilivu.

Shirika hilo linatoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuchukua hatua sasa, “Si tu kwa kukidhi mahitaji ya dharura, bali pia kuwawezesha wanawake kujenga mustakabali wa usawa kwa vizazi vijavyo.”