Ubadilishanaji wa taarifa kwa wakati sahihi utapunguza uhalifu baharini
Ubadilishanaji wa taarifa kwa wakati sahihi utapunguza uhalifu baharini
Panama ambayo inashikilia urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Agosti, imeongoz mjadala wa wazi wa ngazi ya juu kuhusu amani na usalama baharini wakati huu ambapo matukio ya uharamia baharini yanaripotiwa kuimarika tena kwa kutumia teknolojia ya juu.
Miongoni mwa waliohutubia mjadala huo ni Katibu Mkuu wa shirika la Kimataifa la Masuala ya Bahari (IMO), Arsenio Dominguez, ambaye ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na za pamoja duniani kote ili kulinda usalama wa baharini dhidi ya vitisho vinavyozidi kuongezeka, vikiwemo uharamia, mashambulizi ya mtandaoni, na migogoro ya kijiografia.
“Mwaka 2024 pekee, karibu matukio 150 ya uharamia na uporaji kwa silaha yaliripotiwa,” ameonya, akitaja maeneo hatarishi kama vile Lango la Malacca, bahari ya Hindi, na Afrika Magharibi.
Pia amelaani mashambulizi yasiyo halali dhidi ya usafirishaji wa kimataifa katika eneo la baharí ya Sham, akisema yanakiuka sheria za kimataifa na kuhatarisha usalama wa minyororo ya usambazaji duniani.
Licha ya changamoto baharini, shehena zaendelea kusafirishwa
Katibu Mkuu huyo wa IMO amesema licha ya changamoto hizo, mwaka jana pekee zaidi ya tani bilioni 12.3 za bidhaa zilisafirishwa kwa njia ya baharí, wakitegemea mabaharia na watumishi wengine wa baharini wapatao milioni 1.9. “Hii ni hatua nzuri lakini hatua za uimara huu zisiwe sababu za kulegeza juhudi za kuimarisha ulinzi,”
Dominguez ametaja mipango muhimu inayoendeshwa na IMO ikiwemo kanuni za usalama zenye masharti ya lazima, miongozo ya usalama wa mtandao, na makubaliano ya ushirikiano wa kikanda kama vile Kanuni ya Djibouti na Kanuni ya Yaoundé.
Ushirikiano wa kimataifa ni jawabu
Amesifu ushirikiano na mashirika kama UNODC, INTERPOL, pamoja na nchi wafadhili kwa kusaidia ujenzi wa uwezo kupitia miradi kama Bahari Salama kwa Afrika na Mradi wa Kukabiliana na Migogoro ya Bahari ya Sham.
“Usalama wa baharini si suala la kiufundi pekee — ni la kibinadamu kwa kiwango kikubwa,” amesema, akihimiza nchi wanachama wa IMO kuzingatia viwango vya kimataifa na kusisitiza kuwa “ushirikiano wa kimataifa ni msingi muhimu” wa kuwalinda mabaharia na kuhakikisha usafiri salama baharini.
Kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia kama usafirishaji wa kidijitali na meli zinazojiendesha zenyewe, Dominguez pia amesisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu imara ya usalama wa mtandaoni, sambamba na uhifadhi wa mazingira ya baharini.
“Bahari inatuunganisha sote,” amesema huku akikumbusha kuwa “usafirishaji — na maisha ya mabaharia — vinategemea ahadi yenu ya pamoja ya kuhakikisha usalama wa safari baharini.”
INTERPOL inafanya nini kukabili uhalifu baharini?
Katibu Mkuu wa shirika la kimataifa la polisi, INTERPOL, Valdecy Urquiza, ametaka kuchukuliwa hatua za haraka na za pamoja duniani kote ili kutafsiri ahadi za kisheria zilizoko kuwa hatua halisi za kiutendaji katika mapambano dhidi ya uhalifu baharini.
Akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kwenye Mjadala wa Wazi wa Ngazi ya Juu leo Jumatatu kujadili Amani na Usalama duniani, hususan usalama baharini, Urquiza ameonya kuwa “mitandao ya kihalifu inatumia kila mwanya uliopo baina ya mamlaka na kila udhaifu katika ushirikiano wetu.”
Ahadi ziwe vitendo
Katibu Mkuu huyo wa INTERPOL akizungumza kwenye mkutano huo ulioitishwa na Panama, ambayo ndio inashikilia Urais wa Baraza kwa mwezi huu wa Agosti, amesisitiza kwamba ingawa kuna mifumo ya kisheria na ahadi za kisiasa tayari, “kinachohitajika kwa dharura ni utekelezaji unaoleta vyote hivyo mstari wa mbele kupitia ushirikiano wa kimataifa.”
Akieleza nafasi ya INTERPOL kama taasisi huru ya kimataifa, Urquiza amesema shirika hilo linaunganisha vyombo vya sheria kutoka nchi wanachama 196 kupitia mfumo salama wa mawasiliano na kanzidata 19 ambazo zina zaidi ya rekodi milioni 150 za kihalifu na hutumika zaidi ya mara bilioni 8 kwa mwaka.
Mkuu huyo wa INTERPOL amesema kanzidata ya Usalama wa Baharini ya shirika hilo, inakusanya taarifa za kiintelijensia kwa wakati halisi kuhusu vitisho vya baharini, shughuli za meli, na mitandao ya uhalifu wa kimataifa.
“Mfumo huu unaungwa mkono na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2634 na 2608, na huwezesha kugundua vitisho mapema na kuvizuia,” amesema afisa huyo.
Kanzidata yafanikisha kunaswa kwa mhalifu Panama
“Wiki iliyopita tu, utafutaji katika Kanzidata ulisaidia polisi nchini Panama kumtambua kiongozi wa mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya bahari kwenda Ulaya, akiwa amezificha kwenye shehena ya kibiashara ya mvinyo,” ameeleza Urquiza, akiongeza kuwa “huo ndio uthabiti wa kuwa na taarifa sahihi kwa wakati muafaka — sehemu ndogo tu ya taarifa inaweza kuwa tofauti kati ya mafanikio na fursa iliyopotea.”
Afisa huyo ametaja taarifa za wakati kuwa ni mojawapo ya nguzo kuu tatu za kuhakikisha usalama wa baharini. Nyingine ni msaada wa pamoja wa kiutendaji na uchunguzi, na uenezaji wa utaalamu wa kimataifa.
“Hakuna nchi yoyote inayopaswa kukabiliana na uhalifu wa baharini peke yake — au bila kuwa na rasilimali zinazolingana na ujanja wa vitisho vya kisasa,” amehitimisha.