Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Burundi walioingia Tanzania 1972 watakiwa kujitokeza kufanyiwa tathmini

Wakimbizi wa Burundi walioingia Tanzania 1972 watakiwa kujitokeza kufanyiwa tathmini.
© UNHCR Tanzania Wakimbizi wa Burundi walioingia Tanzania 1972 watakiwa kujitokeza kufanyiwa tathmini.

Wakimbizi wa Burundi walioingia Tanzania 1972 watakiwa kujitokeza kufanyiwa tathmini

Wahamiaji na Wakimbizi

Moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo wakimbizi pale wanapokaa nchi waliyopatiwa uhifadhi kwa muda mrefu ni kukosa nyaraka muhimu za utambulisho. Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi UNHCR limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanapata suluhu ya changamoto hii.

Juhudi kama hizo zinaendelea hivi sasa huko katika kambi ya wakimbizi ya Katumba iliyoko wilayani Kasulu katika Mkoa wa Kigoma, magharibi mwa Tanzania ambako kunafanyika tathmini ya kina kuhusu ulinzi na kutafuta suluhu ya pamoja kwa wakimbizi wa Burundi.

Akiwa amesimama katika mnara huko Katumba Afisa mawasiliano wa UNHCR Maimuna Mtengela anasema “ mnara huu ni alama ya shukrani kutoka kwa wakimbizi wa Burundi wa mwaka 1972. Wengi wa wakimbizi hawa walipata uraia kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wao ni raia wa kuandikishwa.”

Mtengela anasema pamoja na kwamba watu wengi walipata uraia, lakini bado kuna sehemu ya makundi ya wakimbizi wenye asili ya mwaka 1972 ambao hawana uraia na wanaishi katika makazi ya Mishamo, Katumba na Ulyankulu.

Katika kuhakikisha watu hao wanasaidiwa vyema kwa mujibu wa sheria, afisa huyo wa UNHCR anasema wao pamoja na Serikali ya Tanzania wapo hapo kusaidia wakimbizi wa Burundi.

“ Tupo kwenye makazi ya Katumba tukiendesha zoezi la tathmini ya mahojiano ya kina kwa wakimbizi wa Burundi wenye asili ya mwaka 1972 wanaoishi kwenye makazi haya na hawana suluhisho la kudumu. Hivyo basi, wewe kama ni mkimbizi wa kutoka Burundi na una asili ya mwaka 1972 tafadhali mjulishe mwengine juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi hili.”

Zoezi hilo limeshaanza kwenye makazi ya Katumba na baada ya Katumba wataendelea na Mishamo na Ulyankulu.