Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuuawa kwa waandishi wa habari 6 Gaza, viongozi wa mashirika ya UN walaani

Mwandishi wa habari wa Palestina, Sami Shehada alipoteza mguu wake katika shambulio huko Gaza. (Maktaba)
UN News
Mwandishi wa habari wa Palestina, Sami Shehada alipoteza mguu wake katika shambulio huko Gaza. (Maktaba)

Kuuawa kwa waandishi wa habari 6 Gaza, viongozi wa mashirika ya UN walaani

Haki za binadamu

Kufuatia kuuawa kwa waandishi sita wa habari huko Gaza, viongozi wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa wamekosoa vikali shambulio hilo lililotekelezwa na majeshi ya Israel usiku wa kuamkia leo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amelaani shambulio la anga la Israel tarehe 10 Agosti katika Jiji la Gaza lililosababisha vifo vya waandishi wa habari sita wa Kipalestina, na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na usio na upendeleo. Amesema kuwa takribani waandishi wa habari 242 wa Kipalestina wameuawa tangu vita kuanza na kusisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kuheshimiwa, kulindwa, na kuruhusiwa kufanya kazi zao bila woga au unyanyasaji.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kupitia ukuraza wake wa X imeliita tukio hilo la kuwashambulia kwa ndege isiyokuwa na rubani waandishi wa habari wapatao sita waliokuwa kwenye hema karibu na Hospitali ya  al-Shifa katika jiji la Gaza kuwa ni uvunjifu mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa na wameitaka Israel kutekeleza wajibu wake wa kulinda raia, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) pia limeonesha kusikitishwa sana na tukio hili. Othman Belbeisi, Mkurugenzi wa IOM Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, amenukuliwa akisema, “Uandishi wa habari si uhalifu” na kwamba IOM iko bega kwa bega na waathirika.

Naye Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini, ameyaelezea mauaji haya yaliyopora maisha ya waandishi wa habari watano wa Al Jazeera na mwingine mmoja wa kujitegemea kuwa jeshi la Israel linazima sauti zinazoripoti ukatili kutoka Gaza. Ameeleza pia kwamba vifo hivi vya sasa vinafanya idadi ya waandishi waliouawa Gaza kuwa zaidi ya 200 vita vilipoanza Oktoba 2023.

Lazzarini amesema, “waandishi wa habari wanapaswa kulindwa na pia  vyombo vya habari vya kimataifa viweze kuingia Gaza kusaidia kazi ya kishujaa ya wenzao Wapalestina. Hii ndiyo njia pekee ya kupambana na uongo na kuzuia mashaka kuhusu ukubwa wa ukatili unaotendeka Gaza.”

Tukio hili la Israel kuwaua waandishi wa habari limekuja saa chache tu baada ya Baraza la Usalama kukutana kwa dharura jana Jumapili Agosti 10 kujadili uamuzi wa baraza la mawaziri la Israel wa kuendeleza tena operesheni yake ya kijeshi ndani ya Ukanda wa Gaza na kuchukua udhibiti kamili jiji la Gaza.

Waandishi wa habari wa Al Jazeera waliouawa wametajwa kuwa ni Anas Al-Sherif, Mohammed Qreigeh, Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal, Moamen Aliwa na Mwandishi wa habari wa kujitegemea Mohammad al-Khaldi.