Kila uchao Gaza, msemo wa ‘jana bora kuliko leo’ wadhihirika
Kila uchao Gaza, msemo wa ‘jana bora kuliko leo’ wadhihirika
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya hii leo kuwa hali ya kibinadamu huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli inazidi kuwa mbaya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kutoka Gaza, maafisa hao wamezungumzia hospitali zilizojaa wagonjwa kupndukia, watoto wenye utapiamlo mkali na raia walio dhaifu wanaojitolea kufa ili tu waweze kupata chakula kwa ajili ya familia zao.
Olga Cherevko, ambaye ni afisa kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Dharura, (OCHA) ameelezea kuwa hali katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis ni “ya kushtua” kwani alipofika hapo siku ya Ijumaa wodi za wagonjwa zilikuwa zimejaa pomoni halikadhalika shoroba za hospitali hiyo.
Amesema idadi kubwa ya wagonjwa walikuwa wamehamishiwa hospitali hiyo kutoka vituo vya kijeshi vya kugawa misaada au kutoka barabara yanayopita misafara.
“Kila mtu ambaye anajaribu kupata chakula kwa ajili ya familia yake…na watu hawa wanaendelea kuuawa au kujeruhiwa,” amesema.
Utafutaji wa chakula kwa hali ya kukata tamaa
Afisa huyo wa OCHA amesema alishuhudia watu watano waliokuwa wamejeruhiwa na maiti watatu wakifikishwa hospitalini kwa ajili ya kuhifadhiwa kutoka maeneo ya mgao wa chakula.
Amesimulia pia kuhusu wanandoa vijana aliokutana nao, ambao jitihada zao za kutafuta unga zilikatizwa kwa msiba, baada ya mume kujeruhiwa na mashambulizi.
“Hii ndiyo mara ya kwanza na ya mwisho mkewe atamruhusu afanye jambo kama hili,” Bi. Cherevko amesema, akiongeza kuwa raia sasa “hawana njia nyingine yoyote” ya kuepuka njaa.
Na wodi ya watoto kwenye Hospitali ya Nasser ilikuwa imejaa wagonjwa waliokosa lishe, na hata watu wazima waliokuwa wamejeruhiwa walikuwa “wamezorota kabisa kiafya, wembamba wa kutisha, na wenye njaa kali mno.”
Amesisitiza kuwa, “kitu pekee tunachohitaji kwa dharura sasa ni usitishaji wa kudumu wa mapigano,” kwani janga hili limefikia “viwango vya kutisha visivyofikirika.”
Uhaba wa sukari
Akihiro Seita, Mkurugenzi wa Afya wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina (UNRWA), ameeleza hali nyingine ya kusikitisha: hakuna kabisa sukari, matunda, au vyakula vyenye sukari Gaza.
Amesema bei zimepanda hadi kufikia dola 100 kwa kilo, akibainisha kuwa kwa watoto wenye ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza, ukosefu wa sukari unafanya kuwa vigumu kutibu hypoglycaemia au kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini.
“Kitu ambacho katika hali ya kawaida hakingekuwa shida sasa ni hatari ya kifo Gaza,” amesema, akitaja kama “ukatili usiovumilika.”
Pia ameeleza kuwa virutubisho maalum kwa watoto waliodhoofika kimwili vimekwisha, akitaja ripoti kutoka mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kuwa shehena za hivi karibuni zimeisha au kuporwa na watu waliokuwa katika hali ya uhitaji mkubwa.