GAZA: Baraza la Usalama la UN lakutana Jumapili kwa kikao cha dharura
GAZA: Baraza la Usalama la UN lakutana Jumapili kwa kikao cha dharura
“Uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Israel unahatarisha kuchochea sura nyingine ya kutisha katika mzozo huu, ambayo inaweza kuwa na madhara makubwa hata nje ya Israel na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu,” amesema Miroslav Jenča, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Ulaya, Asia ya Kati na Amerika.
Amesema hayo wakati akihutubia Baraza la Usalama lililokutana leo Jumapili Agosti 10 kwenye kikao cha dharura kujadili uamuzi wa baraza la mawaziri la Israel wa kuendeleza tena operesheni yake ya kijeshi ndani ya Ukanda wa Gaza na kuchukua udhibiti kamili jiji la Gaza.
Bwana Jenča katika hotuba yake yenye kurasa nne ameeleza kuwa mnamo tarehe 8 Agosti, Baraza la Usalama la Israel liliripotiwa kuidhinisha mpango uliopendekezwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa “kuishinda Hamas”, likipitisha pia kanuni tano za kumaliza vita.
Kanuni 5 za Israel
Kanuni hizo ni: kuondoa silaha za Hamas, kuachiliwa kwa mateka wote, kuondolewa kwa shughuli za kijeshi katika Ukanda wa Gaza, Israel kuwa na udhibiti wa kiusalama katika eneo hilo, na kuanzishwa kwa utawala mbadala wa kiraia usio Hamas wala Mamlaka ya Palestina.
Aidha, ametaja tangazo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu likisema kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litaanza maandalizi ya kuchukua udhibiti wa Jiji la Gaza, huku likitoa misaada ya kibinadamu nje ya maeneo ya mapigano.
IDF imesema kuwa imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuanzisha operesheni ya kijeshi iliyopanuliwa ndani ya Gaza. “Hii ni hatua nyingine hatari ya kuongeza mzozo huu,” ameonya, lakini akaongeza: “Hadi sasa, tuna taarifa chache rasmi kuhusu mipango ya kijeshi ya Israel.”
Mipango ya Israel
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel, serikali inapanga kuwahamisha raia wote kutoka Jiji la Gaza kufikia tarehe 7 Oktoba 2025, hatua itakayowaathiri watu takriban 800,000, wengi wao wakiwa tayari walishawahi kuhama.
Ripoti zinaeleza kuwa IDF itazunguka jiji hilo kwa kipindi cha miezi mitatu, kisha ifuate miezi miwili zaidi ya kudhibiti kambi za Gaza ya kati na kusafisha eneo lote dhidi ya vikundi vya wapiganaji wa kipalestina.
Bwana Jenča ameonya kuwa “iwapo mipango hii itatekelezwa, huenda ikasababisha janga jingine kubwa Gaza, likisambaa katika ukanda mzima na kuleta uhamishaji wa lazima wa watu, vifo na uharibifu zaidi — hali ambayo itaongeza mateso yasiyovumilika kwa raia wa Gaza.”
Ametoa wito wa sitisho la kudumu la mapigano, kuachiliwa kwa haraka na bila masharti kwa mateka wote, na Israel iheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
Watumishi 500 wa kiutu wameuawa Gaza tangu Oktoba 2023
Ramesh Rajasingham, ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) huko Geneva Uswisi na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu, amehutubia pia wajumbe wa Baraza kuhusu kile kinachoendelea Gaza.
“Ninasikitishwa sana na kuendelea kwa mzozo huu na madhara zaidi kwa binadamu ambayo huenda yakatokea kufuatia uamuzi wa serikali ya Israel ya kupanua operesheni zake za kijeshi huko Gaza,” amesema Rajasingham.
Ameongeza kuwa “hii ni hatua ya hatari sana katika mzozo ambao tayari umeleta mateso yasiyoelezeka.”
Rajasingham pia ameeleza kwa masikitiko idadi kubwa ya watumishi wa kibinadamu waliouawa Gaza akisema, “wafanyakazi zaidi ya 500 wa misaada ya kibinadamu wameuawa Gaza tangu mapigano yaanze, miongoni mwao wanawake 167.”
Amesema mashambulizi dhidi ya huduma za kiutu yanasikitisha na kwamba, “tunapokaribia Siku ya Kimataifa ya Wahudumu wa Misaada ya Kibinadamu, ni lazima tusisitize juu ya ulinzi wa wafanyakazi wote wa misaada.”.