Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukizi ya Nagasaki iende sambamba na vitendo vya kutokomeza nyuklia – Guterres

Mji wa Nagasaki ulivyobaki baada ya kudondoshwa bomu la Atomiki, hapo ni umbali wa mita 700 kutoka kitovu cha mlipuko, kama ulivyoonekana  tarehe 10 Agosti 1945.
UN Photo/Yosuke Yamahata
Mji wa Nagasaki ulivyobaki baada ya kudondoshwa bomu la Atomiki, hapo ni umbali wa mita 700 kutoka kitovu cha mlipuko, kama ulivyoonekana tarehe 10 Agosti 1945.

Kumbukizi ya Nagasaki iende sambamba na vitendo vya kutokomeza nyuklia – Guterres

Amani na Usalama

Siku kama ya leo Agosti 9, miaka 80 iliyopita, saa 5 na dakika 2 za asubuhi kwa saa za Japan, Marekani iliangusha bomu la atomiki jijini Nagasaki katika kisiwa hicho kilichoko baharí ya Pasifiki na kusababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na wengine hadi leo hii wakihaha na madhara ya bomu hilo.

Ni kutokana na madhara ya wakati ule na yanayoendelea kukumba manusura ambao kwa kijapani huitwa, Hibakusha, ndio maana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametumia hotuba yake ya siku hii ya kumbukizi kusema kuwa dunia isiyo na silaha za nyuklia inawezekana.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Msadizi wake anayehusika na masuala ya kutoeneza silaha, Izumi Nakamitsu, Guterres amesema licha ya taswira inayoonekana na mvutano katika silaha za nyuklia, bado kuna matumaini ya kuondokana nazo.

Sanamu ya Amani ya kumbukumbu ya shambulio la bomu la nyuklia huko Nagasaki nchini Japan. Eneo hili ni mahsusi kwa masuala ya amani.
UN News/Pengfei Mi

Tunakumbuka maelfu ya watu waliopoteza maisha ghafla, na kuomboleza pamoja na wale waliopoteza wapendwa wao. Natambua uwepo wa hibakusha ambao ujasiri wao na ushuhuda wao vimebaki kuwa dira ya maadili ya kudumu kwa ulimwengu,” amesema Guterres.

Amesifu wakazi wa Nagasaki kwa ujasiri wao wa kujenga upya jiji lao kutoka kwenye magofu hadi kuwa mji wa amani, utamaduni, na uhusiano wa kimataifa. "Nagasaki ni taa ya matumaini kwa dunia," amesema.

Kumbukizi ya Nagasaki sambamba na kuanzishwa kwa UN

Kumbukizi ya shambulio la Nagasaki la mwaka 1945, linaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 80 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, taasisi iliyoasisiwa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kwa lengo la kuzuia vita siku zijazo.

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia kulikuwa ajenda ya kwanza kabisa ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jambo linaloonesha uzito wa suala hilo tangu awali.

Hata hivyo, ameonya kuwa kivuli cha silaha za nyuklia kimerudi tena, zikionekana kuwa sehemu ya mikakati ya usalama wa mataifa, na wakati huo huo matumizi ya kijeshi yamepanda hadi viwango vya juu vya kihistoria, huku uwekezaji katika amani na maendeleo endelevu ukididimia.

Nuru ya kutokomeza nyuklia iko dhahiri

Pamoja na changamoto hizo, Katibu Mkuu ametaja ishara za matumaini, ikiwa ni pamoja na tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2024 iliyotolewa kwa Nihon Hidankyo, shirika la Kijapani linalowakilisha hibakusha ambao ni manusura wa mabomu ya Hiroshima na Nagasaki.

Pia amekumbusha kuwa katika Mkataba wa Zama Zijazo uliopitishwa mwaka jana, mataifa yalijitolea tena kwa dunia isiyo na silaha za nyuklia.

Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani  ya UN, jijini New York, Marekan
UN/Jihye Shin

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana kupitia mashindano ya silaha. Hivoy ametoa wito kwa mataifa kurejea kwenye mbinu zilizothibitishwa za kudhibiti silaha kama vile mazungumzo, diplomasia, kujenga imani, uwazi, na mikataba ya upunguzaji wa silaha.

Amehimiza pia kuimarishwa kwa mfumo wa kimataifa wa kutokomeza silaha, ukiwa na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT) kama msingi, pamoja na kuungwa mkono na Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia (TPNW).

"Tuwaheshimu waathiriwa wa Nagasaki si kwa kumbukumbu tu, bali kwa azimio. Tukumbuke yaliyopita ili tujenge leo na kesho yenye amani," amesema huku akitoa wito kwa jamii ya kimataifa, "tufanye kazi pamoja na kwa haraka kwa ajili ya dunia isiyo na silaha za nyuklia."

Hotuba ya Guterres kwa Mameya waliokutana Nagasaki

Mapema akihutubia kwa njia ya video mkutano wa mameya huko Nagasaki, Katibu Mkuu amesema miaka 80 baada ya Marekani kurusha mabomu mawili ya atomiki katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japani, "uhakika pekee" wa kuzuia matumizi ya silaha za nyuklia leo ni kuziondoa kabisa.

Akiwa amehamasishwa na hibakusha ambao wamegeuza mateso yao kuwa wito wenye nguvu wa amani Guterres amerejelea wito wake wa dunia isiyo na silaha za nyuklia kupitia ujumbe wa video kwa Mkutano Mkuu wa 11 wa Mameya kwa Ajili ya Amani uliofanyika Nagasaki.

Wakiwa wameshikamana pamoja dhidi ya silaha za nyuklia, mkutano huo wa mameya umekuwa ni fursa kwa mameya kutoka kote duniani kujadili na kupitisha vipaumbele muhimu katika kuunga mkono juhudi za kimataifa za kuondoa silaha za nyuklia.