Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu, mamilioni ya watu hatarini - Edem Wosornu

Edem Wosornu, Mkurugenzi wa Operesheni wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA.
© UNOCHA/ Samreen Abuidris
Edem Wosornu, Mkurugenzi wa Operesheni wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA.

Sudan inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu, mamilioni ya watu hatarini - Edem Wosornu

Amani na Usalama

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kutoka Sudan leo (8 Agosti), Mkurugenzi wa Operesheni wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA, Edem Wosornu, amesema, “nilichokiona Khartoum kilikuwa cha kusikitisha sana. Ilikuwa ni jiji lililoharibika vibaya, Khartoum ambayo hapo awali ilikuwa na shamrashamra za maisha, sasa ni kama mji wa mizimu, jiji lililoangamizwa kabisa.”

Wosornu ameeleza waandishi waliokuwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kuwa alitembelea ofisi za OCHA mjini Khartoum na akabainisha kuwa timu haikuweza kuingia ndani ya majengo hayo “kwa sababu ya mabaki ya vilipuzi ambavyo havijalipuka, mabaki ya vita ambayo hayajasafishwa na Huduma za Umoja wa Mataifa za kuondoa vilipuzi, ambazo zimekuwa zikisafisha ofisi mbalimbali kote jijini.”

Amesema, “sijawahi kuona kitu kama hiki katika karibu robo karne ya utumishi wangu kwa Umoja wa Mataifa na kwa shughuli za kibinadamu, katika mazingira magumu na yenye vita. Hii ndiyo hali mbaya zaidi niliyowahi kushuhudia.”

Kuhusu ufadhili, afisa huyo wa masuala ya kibinadamu amesema, “tunachoomba kimsingi ni senti 55 kwa siku kwa kila mtu nchini Sudan. Na basi. Tukipata fursa ya kufika, tunaweza kusaidia. Tukipata uhakika wa usalama, tunaweza kusaidia. Tukipata vifaa vya kutosha na ufadhili, tunaweza kusaidia.”

Amesema Sudan inakabiliwa na “janga kubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani, mgjanga kubwa zaii la afya, na idadi kubwa zaidi ya watu wanaohitaji msaada.”

Wanawake na wasichana wanafanya safari ndefu kukimbia ghasia katika jimbo la Gedaref nchini Sudan.
© UNFPA
Wanawake na wasichana wanafanya safari ndefu kukimbia ghasia katika jimbo la Gedaref nchini Sudan.

Wosornu ameongeza kuwa, wanapokea asilimia 23 pekee ya kilewalichoomba. “Tumepokea karibu dola bilioni moja na tumefanikiwa kuwasaidia watu milioni 13. Unaona, tukipata msaada, tukipata ufadhili usio na masharti magumu, tunaweza kuchukua hatua haraka. Hakika Shirika la Chakula Duniani (WFP), UNICEF, Shirika la Umoja wa ,Mataifa la Afya Duniani (WHO), UNFPA, IOM, mashirika yote ya Umoja wa Mataifa, pamoja na asasi za kitaifa na kimataifa, wanaweza kuchukua hatua.”

Tangu Aprili 2023, Sudan inakabiliwa na mgogoro wa kibinadamu usio na kifani unaosababishwa na mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF). Raia wanaendelea kubeba mzigo wa vurugu, huku karibu watu milioni 9 wakikimbia makazi yao nchini, na kuifanya Sudan kuwa taifa lenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani. Wengine zaidi ya milioni 3 wamekimbilia nchi jirani.

Takribani theluthi mbili ya wananchi wa Sudan wako katika uhitaji mkubwa wa msaada wa kibinadamu, wakiwemo watoto milioni 16. Ukosefu mkubwa wa chakula umefikia viwango vya kihistoria, huku hali ya njaa ikithibitishwa katika maeneo mbalimbali ya nchi na mamilioni ya watu wako hatarini kufa kwa njaa. Wakati huo huo, milipuko ya magonjwa inaendelea kuzidisha hali ya dharura, sambamba na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.

Wanawake na wasichana wako kwenye hatari zaidi, wakikabiliwa na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono vinavyohusiana na mizozo.