Dola milioni 130 zatakiwa kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu kwa wakimbizi kutoka Darfur
Dola milioni 130 zatakiwa kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu kwa wakimbizi kutoka Darfur
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linatoa wito wa msaada wa haraka wa kifedha (dola milioni 130) ili kuzuia kusambaa zaidi kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaowaathiri wakimbizi kutoka Sudan walioko nchini Chad, pamoja na jamii zinazowahifadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi hii leo Afisa wa masuala ya ulinzi kwa eneola Darfur kutosha UNHCR Jocelyn Elizabeth Knight ameeleza kuwa tangu mwezi Juni, zaidi ya wagonjwa 264 wa kipindupindu wamethibitishwa katika kambi ya Douguia Mashariki mwa Chad, ambako tayari watu 12 wamefariki dunia. Kambi ya Treguine nayo inashukuwa kuwa na wagonjwa.
Knight amesema “Kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa huduma za afya, maji safi, usafi wa mazingira, makazi na lishe ili kuepusha janga la afya ya umma.”
Mbali na Chad, Afisa huyo wa UNHCR ameeleza hali nim baya pia nchini Sudan hususani jimboni Darfur ambako ameeleza wananchi wanakabiliwa na hali mbaya zaidi, ambako zaidi ya wagonjwa 4,300 wa kipindupindu wameripotiwa na zaidi ya vifo 110 vimerekodiwa hadi kufikia mwisho wa Julai.
UNHCR inasema hali hiyo inachochewa na mazingira duni ya usafi, ukosefu wa maji safi na uwepo wa msongamano mkubwa katika makazi ya wakimbizi.
Soma hapa taarifa ya mlipuko wa kipindupindu Sudan
UNHCR inatoa wito kwa wahisani kuharakisha msaada ili kunusuru maisha ya maelfu ya wakimbizi, hususan watoto na wanawake, ambao tayari wanakabiliana na athari za vita na ukimbizi wa muda mrefu.