Pazia la LLDC3 lafungwa Awaza kwa mwelekeo mpya kwa nchi zisizofikiwa na bahari
Pazia la LLDC3 lafungwa Awaza kwa mwelekeo mpya kwa nchi zisizofikiwa na bahari
Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zisizokuwa na bandari za baharini, (LLDCs) umekunja jamvi leo Ijumaa Agosti, 8 huko Awaza, Turkmenistan, ambapo wajumbe wamepitisha tamko la kisiasa la kihistoria lenye lengo la kuharakisha maendeleo endelevu na kuimarisha ustahimilivu wa nchi hizo 32 zisizo na njia ya moja kwa moja ya kufikia bahari.
Ukifanyika chini ya kaulimbiu Kuchochea Maendeleo Kupitia Ushirikiano, mkutano huo wa siku nne – LLDC3 – uliwakutanisha wakuu wa nchi, maafisa waandamizi wa UN, washirika wa maendeleo, na viongozi wa sekta binafsi ili kushughulikia changamoto sugu kama vile gharama kubwa za biashara, miundombinu duni, na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huu ulijikita kwenye Mpango wa Awaza wa Hatua 2024–2034, uliopitishwa na Baraza Kuu la UN mwaka jana. Tamko jipya la "Awaza" linaweka mkakati wa pamoja katika maeneo matano ya kipaumbele:
- Mabadiliko ya kiuchumi ya kimuundo
- Biashara na ujumuishaji wa kikanda
- Usafirishaji na miundombinu
- Mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hatari za majanga
- Uhamasishaji wa fedha na ushirikiano
Kauli za viongozi
“Tamko la Awaza ni hatua ya mabadiliko. Ni mpango wa utekelezaji, si maneno tu,” amesema Naibu Katibu Mkuu wa UN, Rabab Fatima, ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa UN kwa nchi zenye maendeleo duni na visiwa vidogo vinavyoendelea (UN-OHRLLS).
Amesema mkutano huu utabaki kuwa kumbukumbu ya wakati wa mabadiliko katika safari ya LLDCs – mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano madhubuti na hatua thabiti.
Mustakabali ambamo kwao dunia haigawanywi kijiografia, bali “tunaunganishwa kupitia Mawazo, biashara na ubunifu. Hebu na tugeuza hoja ya kuunganishwa kwa ardhi isiwe tu ya kinadharia bali mbinu mpya ya maisha.”
Wito wa Uwekezaji na Ushirikishwaji
Tamko linatoa wito kwa benki za maendeleo za kimataifa, kuongeza uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa nchi zinazoendelea, na kuhusisha kwa mapana masilahi ya LLDCs kwenye ajenda za kimataifa za biashara na tabianchi.
Pia linaangazia umuhimu wa kufuatilia utekelezaji na kuhakikisha LLDCs zenyewe zinaongoza mchakato huo kwa uratibu na UN-OHRLLS.
Nini Kinafuata?
Tamko la Awaza ni hatua kubwa mbele kwa LLDCs na ishara mpya ya mshikamano wa kimataifa – likigeuza changamoto ya jiografia kuwa fursa ya pamoja. Utekelezaji wake utafuatiliwa na Baraza Kuu la UN kupitia mikutano ya mawaziri wa LLDC kila mwaka.
Majukwaa muhimu yajayo kusaidia vipaumbele vya LLDC ni pamoja na:
- Mkutano wa Tabianchi wa UN wa 2025 nchini Brazil (COP30)
- Mkutano ujao wa UN kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD)
- Mkutano wa viongoi wa dunia wa 2027 nchini Kyrgyzstan
Mapitio ya kati ya Mpango wa Awaza yamepangwa kufanyika mwaka 2030.
Ushirikiano unaanzia na majirani
Katika mkutano wa waandishi wa habari wa kufunga, Aksoltan Ataeva, Mwakilishi wa Kudumu wa Turkmenistan katika UN, amesema kwamba kwa nchi yake, “kuwa mwenyeji wa LLDC3 si tu tukio kubwa la kisiasa, bali ni kielelezo cha falsafa ya sera ya kigeni ya Turkmenistan: kuwa daraja, si kizuizi.”
Nchini Lesotho, nchi ya Afrika isiyo na bahari, maji ni rasilimali kuu. Amanda Khozi Mukawashi, Mratibu Mkazi wa UN, amesema Lesotho ina nia ya kushirikiana rasilimali zake kama maji, lakini inahitaji uwekezaji.
“Lesotho ina maji mengi yanayosaidia nchi jirani kama Namibia na Botswana. Wanahitaji miundombinu ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji,” amesema
Ameongeza kuwa Lesotho inaweza pia kutumia upepo na jua kuzalisha nishati, si tu kwa matumizi ya ndani bali pia kwa kuuza kwenye kanda yenye changamoto za nishati na maji.
Kwaheri Awaza
Ijumaa, Awaza – iliyo kwenye mwambao wa Bahari ya Caspian – iliaga wageni wake kwa kushusha rasmi bendera za UN na Turkmenistan zilizokuwa zimepandishwa mwanzoni mwa wiki.
“Awaza itakumbukwa kama hatua ya mabadiliko katika safari ya LLDCs – si tu kwa mafanikio ya mkutano, bali kama mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano thabiti na utekelezaji wa kweli,” amesema Bi. Fatima akihitimisha mkutano huo.