Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo kutoka UNDP Tanzania yafungua macho wakusanyaji wa taka Mtwara

Wanawake na vijana washirikiana kukusanya taka za plastiki kwa ajili ya utunzaji wa mazingira na urejelezaji wa taka huko Mtwara kusini mwa Tanzania.
© UNDP Tanzania
Wanawake na vijana washirikiana kukusanya taka za plastiki kwa ajili ya utunzaji wa mazingira na urejelezaji wa taka huko Mtwara kusini mwa Tanzania.

Mafunzo kutoka UNDP Tanzania yafungua macho wakusanyaji wa taka Mtwara

Wanawake

Huko mkoani Mtwara, kusini mwa Tanzania shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP limeendesha warsha ya siku tatu ya mashauriano kuhusu uchumi rejeshi ili pamoja na mambo mengine kuelimisha vikundi vya wanawake na vijana kuhusu utunzaji wa mazingira na urejelezaji wa taka.

Miongoni mwa walioshiriki ni Hauwa Abdallah Chande, Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake cha Mtwara Kuchele kinachohusika na usafi wa mazingira ambaye anakiri kuwa awali hakujua kuwa taka wanazokusanya na kutupa kama vile chupa ni ‘lulu’.

“Ninashukuru mimi, yaani kuna kitu nimejifunza hasa kuna taka zingine tunatupa bila kujua faida yake. Kwa mfano, hivi vyupa tulikuwa tunavidharau. Sasa semina hii, Nimejifunza kwamba chupa ni mali chuma ni mali,” amesema Bi. Chande ambaye kikundi chake kina wanachama 22.

Akafafanua kuwa kupitia semina, “nimeona leo faida yake kwamba kumbe ukiokota vitu kama hivi ukivitunza, kuna soko maalum unaweza kuuza na kujiendeleza na hela zao unazopata.”

Hauwa Abdallah Chande, Mwenyekiti wa kikundi Mtwara Kuchele.
© UNDP Tanzania
Hauwa Abdallah Chande, Mwenyekiti wa kikundi Mtwara Kuchele.

Anachoenda kufundisha wengine

Kwanza naenda kuwapa elimu moja kwamba chochote tunachookota chupa, chuma tuwe tunatunza kitakuwa faida mara mbili zaidi licha na ajira yetu ya kufyeka mazingira, lakini hizo chupa tutaendelea kupata hela kwa faida yetu sisi wenyewe.

Kikundi chao kilianza miaka 12 iliyopita baada ya kuona uchafu mjini Mtwara. “Tulijitolea  mwaka mzima. Tunatoa michanga kwenye mitaro iliyoziba, Tunatoa mchanga, tunaweka pembeni..”

Hatimaye Manispaa ya Mtwara iliwaona juhudi zao na kuwapatia zabuni ya kusafisha barabara za mjini ambapo Bi. Chande anasema “barabara za mjini zote tunafika na kufagia , tunafanya kazi vizuri na bila unyanyasaji. Na wengine tumejenga nyumba kwa kazi hii.”

Kwa wanakikundi cha mazingira cha Mtwara Kuchele, tabia ya watu kutupa taka hovyo ndio changamoto kuu akisema, “unakuta vyupa, mtu amekojolea mkojo lakini sisi tunapambana tunatoa vile vyupa, tunatia kwenye mifuko, tunapeleka dampo yaani tunajituma bila hiyana bila kuwa na kichefuchefu kwa sababu ile kazi ipo kwenye damu na vifaa vyake vipo. Tunashukuru.”

Fursa ya mikopo

Kwa kuwa kikundi chao kimesajiliwa, Bi. Chande anasema anachoshukuru zaidi ni kwamba kupitia kazi yao na kikundi chao, “ninashukuru mno mikopo kutoka Manispaa. Tunapatiwa na tunarejesha inavyotakiwa na hatuwi wababaishaji.”

Akawa na  ujumbe kwa wakazi wa Mtwara kuhusu utunzaji mazigira akisema, “wawe waelewa wanachoambiwa kitu kwamba chupa usitupe hovyo. Waelewe wazingatie sheria zinazopangwa manispaa.”

Na zaidi ya yote “nawashauri kwamba kazi ya miaka hii kama unajijua hukusoma, umeishia darasa la 7 au darasa 12. Ajira ni ngumu kwa sababu zinaenda kwa awamu. Usichague kazi bali jitume kuokota, jitume, kufyeka. Jitume kutoa michanga kwenye mitaro ni moja ya njia za kupata riziki. Ni hilo tu nawashauri watu wa Mtwara.”