Guterres aiambia Israel; kudhibiti Gaza kutaleta janga kubwa zaidi
Guterres aiambia Israel; kudhibiti Gaza kutaleta janga kubwa zaidi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonesha wasiwasi mkubwa kufuatia uamuzi wa serikali ya Israel wa "kuchukua udhibiti wa mji wa Gaza", eneo la Palestina inalokalia kimabavu, akisema kuwa hatua hiyo ni ya hatari na inaweza kuongeza kwa kiwango kikubwa madhara ambayo tayari ni ya janga kwa mamilioni ya wapalestina.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Ijumaa mchana na msemaji wake jijini New York, Marekani na msemaji wake, Katibu Mkuu amesema kuwa uamuzi huo wa kijeshi unawakilisha hatua mpya ya kutisha katika mzozo huo na unaweza kuhatarisha maisha zaidi, ikiwa ni pamoja na ya mateka waliobaki.
“Wapalestina huko Gaza wanaendelea kukumbwa na janga la kibinadamu la kutisha,” amesema Katibu Mkuu. “Hatua hii mpya ya kijeshi italeta madhara zaidi kama vile kuhamishwa kwa nguvu kwa raia, mauaji, na uharibifu mkubwa – yote haya yakichochea mateso yasiyosemekana kwa watu wa Gaza.”
Mambo 3 kutoka kwa Guterres
Katibu Mkuu amerejea tena wito wake wa haraka wa usitishaji wa kudumu wa mapigano, ufikishaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo kote Gaza, na kuachiliwa huru mara moja na bila masharti kwa mateka wote.
Aidha, Katibu Mkuu ameitaka kwa mara nyingine serikali ya Israel kuheshimu wajibu wake chini ya sheria za kimataifa. Amesisitiza kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kupitia ushauri wake wa tarehe 19 Julai 2024, ilitamka kwamba Israel ina wajibu wa kusitisha mara moja shughuli zote mpya za ujenzi wa makazi ya walowezi, kuwaondoa walowezi wote kutoka katika maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu, na kuhitimisha uwepo wake haramu katika maeneo hayo – yakiwemo Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Yerusalem Mashariki – haraka iwezekanavyo.
Mgogoro utatuliwe kwa njia endelevu
“Tutatue mgogoro huu kwa njia endelevu,” amesema Katibu Mkuu. “Hatuwezi kuwa na suluhisho la kudumu bila kumaliza uvamizi huu haramu na kufanikisha suluhisho la kweli la mataifa mawili.”
Amesisitiza kuwa Gaza ni sehemu muhimu na isiyoweza kutengwa ya taifa la Palestina, na lazima ibaki hivyo kwa mujibu wa sheria na maazimio ya kimataifa.
Israel isitishe mara moja mpango wake - Volker Türk
Mapema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, naye leo alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mpango wa Serikali ya Israel kutwaa kijeshi ukanda wote wa Gaza unaokaliwa kimabavu.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa njia ya video leo Agosti 8 jijini Geneva, Uswisi, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, Liz Throssell ameeleza kwamba, Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk anauona mpango huo wa Israel “unapingana na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ."
Halikadhalika Israel lazima ikomeshe uvamizi wake haraka iwezekanavyo, na unakwenda kinyume na utekelezaji wa suluhisho lililokubaliwa la mataifa mawili na pia haki ya Wapalestina ya kujitawala”.
Anaendelea kueleza kwamba, “kwa ushahidi wote hadi sasa, hatua hii ya kuongeza uvamizi zaidi itasababisha kuongezeka kwa ufurushaji watu, mauaji zaidi, mateso yasiyovumilika, uharibifu usio na maana na uhalifu wa kikatili.”
Vita Gaza vikome
Na kwa msingi huo, “vita vya Gaza lazima vikome sasa. Na waisraeli na wapalestina lazima waruhusiwe kuishi bega kwa bega kwa amani,” anasema Throssel kwa niaba ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.
Amehitimisha “badala ya kuongeza ukali wa vita hivi, serikali ya Israel inapaswa kuelekeza juhudi zake zote katika kuokoa maisha ya raia wa Gaza kwa kuruhusu usambazaji kamili wa misaada usio na vizuizi, makundi yenye silaha ya Kipalestina yawaachie mara moja mateka bila masharti yoyote na. Wapalestina waliokamatwa kiholela na Israel pia wanapaswa kuachiwa mara moja na bila masharti yoyote.”