Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgao wa mlo wavutia wanafunzi Uganda kujifunza zaidi

Uganda. Wafanyakazi wa WFP Uganda na Kenya wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi
@WFP/Siegfried Modola
Uganda. Wafanyakazi wa WFP Uganda na Kenya wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi

Mgao wa mlo wavutia wanafunzi Uganda kujifunza zaidi

Utamaduni na Elimu

Mradi wa mlo shuleni unaotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula(WFP) nchini Uganda kwa kushirikiana na serikali umesaiia zaidi ya watoto 255,000 kuendelea na masomo, kujifunza vizuri zaidi na kustawi. 

Video ya WFP ukanda wa Afrika Mashariki iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram inaanzia kwenye shule ya msingi ya Namalu,wilayani Nakapiripirit kaskazini mwa Uganda.

Ninaona masufuria ya uji wa moto pamoja na wali maharage, huku wanafunzi wakiwa foleni kupokea mgao wa mlo huu.

Grace ni mmoja wa wanafunzi wanufaika wa na anaelezea hali halisi pindi mwanafunzi anapokosa chakula. Anasema "Nimekaa shule ya Msingi Namalu kwa muda wa miaka 6. Wakati wangu ninaoupenda shuleni ni, kuwa darasani. Nitakapokuwa mkubwa nataka kuwa daktari. Ukienda darasani bila kunywa uji au kupata chakula cha mchana, huwezi kuwa sawa darasani, utahisi njaa na hutaelewa kile anachofundisha mwalimu."

Nikiendelea kusalia shuleni hapa,nakutana na Edgar Twinomujuni,yeye ni Afisa Mipango na Sera wa WFP Uganda,anasema, "Eneo hili lina mojawapo ya matokeo mabaya zaidi ya lishe, na hili ni jambo baya sana, hasa kwa elimu. Hivyo, kwa kuwa na programu hii, tumeona maboresho makubwa katika mahudhurio na viwango vya uandikishaji kwa zaidi ya asilimia 15, lakini pia kuboresha matokeo ya lishe katika eneo hili."

Grace anaeleza umuhimu wa mlo shuleni akisema "Kugawa chakula shuleni kunawasaidia watoto. Kwa sababu katika baadhi ya nyumba hawapiki, kama vile chakula cha mchana. Watoto wanakuja wanasoma, wanacheza shuleni, kisha wanapata chakula cha mchana. Ndiyo maana watoto wengine wanakuja shuleni."