WHO: Heshima kwa wajawazito na watoto wachanga ni haki, si hiari
WHO: Heshima kwa wajawazito na watoto wachanga ni haki, si hiari
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limesema kuwa unyanyasaji dhidi ya wajawazito na watoto wachanga bado ni jambo la kawaida katika baadhi ya huduma za afya, na sasa limezindua nyenzo mpya kusaidia kubadili hali hiyo.
Kwa mujibu wa WHO, tafiti katika nchi nne zimeonesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wajawazito walikumbana na kauli za kudhalilisha wakati wa kujifungua, huku zaidi ya asilimia 60 wakifanyiwa uchunguzi katika sehemu za siri bila idhini yao.
Akizungumza katika mahojiano maalum na WHO, Dkt. Chibugo Okoli kutoka Jhpiego nchini Nigeria amesema, “Nimeona mabadiliko chanya yakitokea pale ambapo heshima na utu vinapewa kipaumbele. Lakini pia, kuna changamoto nyingi, hasa mtazamo hasi dhidi ya wanawake wa hali ya chini. Mabadiliko hayawezi kufanikiwa bila kushughulikia mazingira ya kazi na mifumo ya sera.”
Mwongozo wa pamoja
WHO inasema heshima katika huduma si jambo la hiari, bali ni haki ya msingi ya kila mama na mtoto.
Katika kuimarisha huduma zenye heshima, WHO kwa kushirikiana na wadau imechapisha Muongozo mpya unganifu ambao umejumuisha ushahidi muhimu, zana na nyenzo za kusaidia utekelezaji wa kivitendo wa utunzaji wa heshima kwa wazazi na watoto wachanga katika miktadha tofauti
Mwongozo huo unawalenga watoa huduma, wasimamizi wa programu na watunga sera juu ya hatua za kuchukua ili kulinda haki, mahitaji na matakwa ya wanawake na watoto wachanga.
Pia mwongozo huu utasaidia mfumo mzima wa afya, kubuni na kutekeleza huduma zenye staha kwa wote.