Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Hospitali ‘karibu zitashindwa kabisa’, wafanyakazi wa afya wameelemewa na majeruhi

Mvulana anatibiwa majeraha yake katika hospitali ya Al Helou katika mji wa Gaza.
© UNICEF/Rawan Eleyan
Mvulana anatibiwa majeraha yake katika hospitali ya Al Helou katika mji wa Gaza.

Gaza: Hospitali ‘karibu zitashindwa kabisa’, wafanyakazi wa afya wameelemewa na majeruhi

Afya

Wafanyakazi wa misaada wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wamechoka wameendelea kuripoti hadi leo Alhamisi Agosti 7 kuhusu ukosefu wa chakula katika Ukanda wa Gaza, huku timu za matibabu zikiendelea kuonya kuwa hospitali zimeelemewa na majeruhi wanaoingia kila siku na ziko karibu na “kuporomoka kabisa.

Wakati huo huo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yameidhinisha vifo vya Wapalestina watatu waliokufa kwa ugonjwa wa Guillain-Barré Syndrome (GBS), ugonjwa adimu wa kinga mwilini unaoweza kusababisha udhaifu wa ghafla wa misuli hadi kupooza.

Kabla ya vita kuanza Gaza Oktoba 2023, kulikuwa na visa vichache sana vya ugonjwa wa GBS kwa mwaka. Sasa, idadi kubwa ya majeruhi imekuwa jambo la kawaida.

“Hospitali zimeelemewa na matukio ya majeruhi wengi, wastani wa matukio manane kwa siku,” limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada la Umoja wa Mataifa, OCHA, likinukuu wadau wake wengine wa afya.

Mtoto anayeugua utapiamlo amelazwa kwenye kitanda katika Hospitali ya Jamii ya Wagonjwa katika Jiji la Gaza.
© UNICEF/Mohammed Nateel
Mtoto anayeugua utapiamlo amelazwa kwenye kitanda katika Hospitali ya Jamii ya Wagonjwa katika Jiji la Gaza.

Katika taarifa kuhusu hali mbaya ya afya Gaza, OCHA imeeleza kuwa vituo maalum vya urekebishaji wa afya vimeelemewa pia, vikihudumia majeruhi wa kiwewe na visa vya GBS.

Hadi sasa, vifo vitatu kati ya takriban visa 64 vya GBS vimethibitishwa na mamlaka ya afya Gaza, watoto wawili wakiwa ni miongoni mwa waliokufa.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), asilimia 30 ya wagonjwa wa GBS huhitaji uangalizi maalum, lakini hakuna dawa ya msingi ya kutibu, yaani immunoglobulin ya sindano  iliyopo kwa sasa.

Misaada ya kurusha kutoka angani haitoshi

WFP pia imesisitiza wito wake wa kuingiza misaada kwa wingi Gaza, badala ya kiwango kidogo kinachoruhusiwa na mamlaka za Israel.

“Hatuwezi kutegemea misaada ya anga kutatua njaa inayoendelea. Si Gaza,” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Cindy McCain, kupitia chapisho la mitandao ya kijamii Jumatano usiku.

Kiongozi huyo amesema kuwa “watu 500,000 wanakumbwa na njaa leo” na njia pekee ya kuwasaidia ni kuwafikishia chakula kwa wingi kupitia barabara.

“Hatuna muda wa kusubiri; Gaza haina chakula wala muda,” amesema McCain.

Familia moja ikiondoa kifusi kutoka kwa nyumba huko Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Familia moja ikiondoa kifusi kutoka kwa nyumba huko Gaza.

WHO yapoteza ghala la dawa

Uharibifu wa ghala kuu la matibabu la WHO kufuatia shambulio huko Deir Al-Balah mwishoni mwa mwezi uliopita umeathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za kuokoa maisha.

Ukosefu wa dawa muhimu za antibiotiki umetatiza matibabu ya meningitis, ambayo sasa yamefikia mamia ya visa  “idadi kubwa zaidi kurekodiwa tangu kuanza kwa machafuko,” OCHA imesema.

Hatua za kutenga wagonjwa zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na kutenganisha idara ya nje ya Hospitali ya Al Khair kutoka Kituo cha Matibabu cha Nasser, pamoja na kuanzishwa kwa mahema ya kutenga wagonjwa katika Hospitali ya Al Aqsa ili kudhibiti visa vinavyoshukiwa kwa usalama.

Silaha za mlipuko kama mabomu na maguruneti zimetoa asilimia 83 ya mashauriano ya kimatibabu, kwa mujibu wa OCHA.

Taarifa hiyo imenukuu shirika la Madaktari wasio na miaka, Médecins Sans Frontières (MSF), ambalo lilichakata zaidi ya mashauriano ya kimatibabu 200,000 katika vituo sita vya afya vinavyosaidiwa na MSF Gaza mwaka 2024.

Guillain-Barré Syndrome ni nini?

Guillain-Barré Syndrome (GBS) ni ugonjwa wa neva/mishipa mdodgomidogo na kinga mwilini unaoathiri mfumo wa neva na kusababisha kupooza kwa misuli kwa hatua. Sio wa kuambukiza na mara nyingi husababishwa na maambukizi ya virusi au bakteria yaliyopita yanayosababisha mabadiliko katika mfumo wa kinga.

Katika visa vingi, wagonjwa hupata nafuu kamili ndani ya wiki chache. Hata hivyo, WHO imeonya kuwa hata katika mazingira bora ya afya, asilimia 3 hadi 5 ya wagonjwa hufariki kutokana na matatizo ya ugonjwa huu kama kupooza kwa misuli ya kupumua, sepsis, kuganda kwa damu mapafuni, au mshtuko wa moyo.

Kumekuwa na milipuko kadhaa ya magonjwa ya kuambukiza Gaza tangu kuanza kwa vita baada ya mashambulizi ya Hamas nchini Israel, ikiwa ni pamoja na polio, kipindupindu, homa ya ini A, na ukurutu.