Muhtasari wa habari: Wajawazito; Awaza 2025; Gaza
Ushahidi unaonesha kuwa unyanyasaji bado ni jambo la kawaida katika huduma kwa wajawazito na watoto wachanga, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, (WHO) hii leo.
Mathalani katika nchi nne, utafiti umebaini kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wajawazito walikumbana na kauli chafu wakati wa kujifungua ili hali zaidi ya asilimia 60 walifanyiwa uchunguzi sehemu zao za siri bila idhini yao.
Awaza
Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa nchi zisizo na bandari za baharini, LLDCs ukiendelea huko Awaza, Turkmenistan, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP limetaka kubadilika kwa fikra ya kwamba nchi hizo kama vile Rwanda na Uganda zina mkwamo wa kibiashara na maendeleo.
Mwakilishi wa UNDP nchini Ethiopia Dkt. Samuel Doe akizindua mpango mpya wa kuonesha faida za nchi hizo kwa muunganiko wao kwa njia ya ardhi amesema…. hii leo LLDCs zinatumia vema uwepo wao kimkakati, katikati ya Afrika na muunganiko wa kikanda kuwa vitovu muhimu vya kuunganisha nchi kiuchumi , biashara na ubunifu.
Gaza
Na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu leo wamesema ili kuzuia vifo zaidi na mateso kutokana na njaa huko Gaza, Israel inapaswa kurejesha mara moja ruhusa kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kibinadamu kuingia bila vikwazo vyovyote eneo la Palestina inalokalia kimabavu.