Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya raia Kivu Kaskazini mwezi Julai yavunja rekodi- Türk

Thérèse akiwa amembeba mjukuu wake kwenye ua wa nyumba ya familia huko Goma jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNFPA
Thérèse akiwa amembeba mjukuu wake kwenye ua wa nyumba ya familia huko Goma jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mauaji ya raia Kivu Kaskazini mwezi Julai yavunja rekodi- Türk

Amani na Usalama

Volker Türk, ambaye ni Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, amelaani kuongezeka kwa mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na kundi la M23 na makundi mengine yenye silaha dhidi ya raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kwa mujibu wa taarifa za moja kwa moja zilizopokelewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, kati ya tarehe 9 na 21 Julai katika vijiji vinne vya eneo la Rutshuru, katika jimbo la Kivu Kaskazini,  takribani raia 319 waliuawa na waasi wa M23, wakisaidiwa na wanachama wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwamba  mashambulizi haya ya karibuni ni miongoni mwa mashambulizi yaliyosababisha vifo vingi zaidi yaliyowahi kuripotiwa tangu M23 waanze tena harakati zao mwaka 2022.

Amesema “wengi waliouawa, wakiwemo wanawake wasiopungua 48 na watoto 19, walikuwa wakulima wa eneo hilo waliokuwa wakipiga kambi mashambani wakati wa msimu wa kupanda mazao.”

Kumbukeni makubaliano ya kusitisha mapigano

Bwana Türk pia amelaani mashambulizi dhidi ya raia yaliyofanywa na makundi mengine yenye silaha kwani Ofisi ya Haki za Binadamu imeripoti mashambulizi kadhaa katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, na Ituri mwezi Julai, yakiwemo yale yaliyofanywa na makundi ya ADF na CODECO.

Kamishna Mkuu amerejea wito wake kwa pande zote zinazohusika katika migogoro mashariki mwa DRC kuhakikisha ulinzi wa raia dhidi ya madhara, na kuheshimu wajibu wao wote chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Halikadhalika, amezitaka pande zote zilizotia saini tamko la hivi karibuni la misingi kushiriki katika mchakato wa amani kwa nia njema na kuchukua hatua madhubuti za kumaliza mzunguko wa ghasia unaojirudia.