Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

NGOs za misaada kusitisha shughuli zao Gaza iwapo Israel haitofuta masharti mapya

Umoja wa Mataifa hufanya kazi na mashirika kadhaa ya ndani huko Gaza katika kwa kazi kama chanjo dhidi ya polio.
© UNICEF/Eyad El Baba
Umoja wa Mataifa hufanya kazi na mashirika kadhaa ya ndani huko Gaza katika kwa kazi kama chanjo dhidi ya polio.

NGOs za misaada kusitisha shughuli zao Gaza iwapo Israel haitofuta masharti mapya

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya misaada hii leo Jumatano yameonya kwamba mashirika mengi yanayotoa misaada muhimu katika Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel, (oPt) yanaweza kulazimika kusitisha shughuli zao ndani ya wiki chache zijazo, endapo Israel haitafuta agizo linalowataka watoe taarifa nyeti kuhusu wafanyakazi wa kipalestina.

Maendeleo haya – yanayoathiri vibaya pia Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu – ni matokeo ya masharti mapya yaliyowekwa na Israel tarehe 9 mwezi Machi mwaka huu dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa (NGOs).

“Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, mashirika mengi ya misaada ya kimataifa yanaweza kufutiwa usajili ifikapo tarehe 9 mwezi ujao wa Septemba au hata kabla ya hapo – na hivyo kulazimika kuwaondoa wafanyakazi wao wa kimataifa na kushindwa kutoa msaada wa kibinadamu muhimu kwa maisha ya Wapalestina,” umesema Umoja wa Mataifa na mashirika wadau wa  misaada katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu kupitia taarifa iliyotolewa leo.

Mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa bado yanafanya kazi Gaza, yakishirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali kufikia watu walio katika mazingira magumu zaidi.

Mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa yana nafasi muhimu kwa sababu hutoa msaada wa vifaa, fedha, na msaada wa kitaalamu kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kipalestina.

Wito wa pamoja wa mashirika

“Bila ushirikiano huu, shughuli zao zitakatizwa, na jamii nyingi zaidi zitakosa chakula, huduma za afya, malazi na ulinzi muhimu,” imesema timu hiyo ya misaada ya kibinadamu, inayosimamiwa na afisa wa juu wa misaada wa Umoja wa Mataifa katika OPT na inayojumuisha wakuu wa mashirika ya UN na zaidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali  200 ya ndani na ya kimataifa.

Kwa sasa, mashirika ambayo hayajasajiliwa chini ya mfumo huo mpya hayaruhusiwi kutuma msaada wowote kwenda Gaza.

Maombi 29 yalikataliwa

Mwezi uliopita pekee, mamlaka za Israel zilikataa mara kadhaa maombi ya mashirika 29 kutuma misaada ya kibinadamu Gaza, yakiyataja kuwa “hayajaidhinishwa.”

“Sera hii tayari imesababisha kuzuiwa kwa misaada ya kuokoa maisha kama vile dawa, chakula, na vifaa vya usafi,” limesema kundi hilo la mashirika ya misaada.
“Athari zake kubwa zinaonekana kwa wanawake, watoto, wazee, na watu wenye ulemavu, hali inayoongeza zaidi hatari ya kunyanyaswa na ukatili wa kingono.”

Katika taarifa yake, timu hiyo ya pamoja ya usaidizi imetoa wito kwa Israel kuangalia upya agizo hilo la kutaka taarifa nyeti kuhusu wafanyakazi wa kipalestina kutoka mashirika ya misaada yasiyo ya kiserikali, ikisisitiza kuwa kuzuia kazi ya misaada ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.