Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 80 tangu bomu kuangushwa Hiroshima, Guterres asifu mnepo wa hibakusha

Eneo la Hifadhi ya Amani huko Hiroshima, Japan
UN Japan/ Ichiro Mae
Eneo la Hifadhi ya Amani huko Hiroshima, Japan

Miaka 80 tangu bomu kuangushwa Hiroshima, Guterres asifu mnepo wa hibakusha

Amani na Usalama

Katika kumbukumbu ya miaka 80 tangu kutokea kwa shambulio la bomu la nyuklia kwenye mji wa Hiroshima, nchini Japani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma ujumbe mzito wa akisisitiza umuhimu wa amani, kutokomeza silaha za nyuklia, na kuenzi maisha ya waliopotea na walionusurika.

Tarehe 6 Agosti mwaka 1945 Marekani iliangusha bomu la atomiki kwenye jiji la Hiroshima lililosababisha vifo vya watu 80,000 huku makumi ya maelfu wakikumbwa na miali ya nyuklia. Siku tatu baadaye, yaani Agosti 9, bomu la pili la nyuklia liliangushwa na Marekani huko mjini Nagasaki.

Dunia ilibadilika milele

“Miaka 80 iliyopita siku kama ya leo, dunia ilibadilika milele,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa,  “Kwa muda wa sekunde chache, jiji la Hiroshima liliteketezwa kwa moto. Maelfu walipoteza maisha. Jiji likawa magofu. Na ubinadamu ulivuka mpaka ambao haungeweza kurudi nyuma.”

Katika hotubayake iliyosomwa kwa niaba na Msaidizi wake Izumi Nakamits, Katibu Mkuu amewakumbuka wale waliopoteza maisha na kuelezea mshikamano na familia ambazo hadi leo zinabeba kumbukumbu hiyo chungu. Pia amesifu ujasiri wa hibakusha – yaani manusura wa mabomu ya Hiroshima – akisema sauti zao zimekuwa nguzo ya maadili katika juhudi za kulinda amani duniani.

“Ingawa idadi yao inapungua kila mwaka, ushuhuda wao na ujumbe wao wa kudumu wa amani hautatuacha kamwe,” amesema Katibu Mkuu.

Mnepo wa Hiroshima

Akiangazia ustahimilivu wa watu wa Hiroshima, Katibu Mkuu amesema wengi walidhani jiji hilo halingeweza kupona wala kiumbe chochote kuota tena, lakini wakaazi wamevunja matarajio hayo.

“Hamkujenga tu jiji. Mlijenga tena matumaini. Mliotesha maono ya dunia isiyo na silaha za nyuklia, na mkayashirikisha ulimwengu mzima.”

Katika mfano wa matumaini hayo, mwezi Mei miche ya miti iliyooota kutoka kwenye mbegu za miti iliyosalia baada ya bomu ilipandwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini  New York , Marekani – kama ishara ya ushindi wa roho ya mwanadamu na jukumu la pamoja la kulinda vizazi vijavyo dhidi ya maangamizi ya nyuklia.

Katibu Mkuu pia amekumbusha kwamba mwaka huu pia ni maadhimisho ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, chombo kilichoanzishwa kwa dhamira ya kuzuia vita, kulinda utu wa binadamu, na kuhakikisha kwamba majanga ya zamani hayajirudii tena.

Hata hivyo, ameeleza wasiwasi wake kuwa hatari ya mzozo wa nyuklia inaongezeka tena, uaminifu kati ya mataifa unazidi kudhoofika, na migawanyiko ya kisiasa inakua kwa kasi.

“Silaha zile zile zilizoharibu Hiroshima na Nagasaki nchini Japan sasa tena zinachukuliwa kama nyenzo za kutishia.”

Dalili za matumaini

Ingawa hivoy amesema kuna dalili za matumaini. Amelitaja shirika la Kijapani la Nihon Hidankyo, linalowakilisha manusura wa Hiroshima na Nagasaki, ambalo lilitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2024 kutokana na kazi yake ya kuelimisha kuhusu hatari za silaha za nyuklia.

Pia ametaja Mkataba wa Zama Zijazo uliopitishwa mwaka 2024 na nchi wanachama wa UN, ambapo nchi zilikubaliana upya kujenga dunia isiyo na silaha za nyuklia.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa ahadi lazima ziende sambamba na hatua za kweli, hususan kupitia kuimarisha Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na kuendeleza kasi iliyochochewa na Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia (TPNW).

Amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa mataifa akisema, “Tuvute nguvu kutoka kwa ustahimilivu wa Hiroshima na hekima ya hibakusha. Tufute tishio la silaha za nyuklia kwa kuzifuta kabisa. Tutimize ahadi yetu kwa hibakusha, na kuhakikisha ushuhuda wao na ujumbe wa amani unarithiwa na vizazi vijavyo.”

Guterres amesema kukumbuka yaliyopita ni kulinda na kujenga amani ya leo — na ya kesho.