UN yarejelea wito wa kutaka kuachiliwa huru kwa mateka wa Israeli huko Gaza
UN yarejelea wito wa kutaka kuachiliwa huru kwa mateka wa Israeli huko Gaza
Ikiwa ni siku 668 tangu Hamas ambao ni wanamgambo wa kipalestina wateke waisraeli 250 baada ya kushambulia taifa hilo la Mashariki ya Kati, vuta nikuvute ilikuwa bayana kwenye Baraza la Usalama baada ya kikao cha dharura kuitishwa na Israeli Jumanne Agosti 5, kufuatia kuchapishwa kwa picha za mateka wawili walio hoi bin taaban.
Mkutano ulifanyika kuanzia saa 9 alasiri kwa saa za New York, Marekani kwa takribani saa mbili na dakika 50, Umoja wa Mataifa ukiwakilishwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu kwa masuala ya ulaya, Asia ya Kati na Amerika Miroslav Jenča.
Amezungumzia picha hizo zikiwemo za Evaytar David na Rom Braslavsky waliodhoofika akisema mandhari ya Evaytar akishinikizwa kuchimba kaburi lake mwenyewe zinatisha. Sheria ya Kimataifa iko wazi. Uchukuaji watu mateka hauruhusiwa – ni uhalifu wa kivita. Lazima waachiwe huru sasa.”
Kaka yangu yuko mifupa mitupu
Ilay David, ambaye ni kaka yake Evyatar David, akihutubia wajumbe wa Baraza kwa njia ya video amesema “kaka yangu alikuwa kama mfupa iliyo hai. Hakuwa na nguvu za kutembea wala kuzungumza. Tunakumbushwa ni kwa kiasi gani Hamas na washirika wao ni wakatili na wasio na ubinadamu.”
David ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia mateka, akisema, “wakati misaada inaendelea kuingia Gaza kuwasaidia wakazi, mateka wananyimwa hata mahitaji ya msingi ya maisha. Hawajawahi kupokea hata tone la msaada wa kibinadamu tangu walipotekwa. Huu ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa,”.
Kulikoni mateka wetu wananyimwa huduma?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar, yeye akahoji kwa nini mateka hao hawapatiwi huduma za lishe na matibabu “wakati magaidi, wauaji, wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israeli wanapatiwa huduma ya matibabu na lishe, Hamas na kikundi cha Jihadi wanatesa mateka wetu.”
Hakuna cha kuhalalisha tukio la 7 Oktoba na baada ya hapo
Kwa Riyadh Mansour, Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa akafunguka, "Tunaelewa wazi kwamba kile ambacho Israeli ilifanya kabla ya tarehe 7 Oktoba hakiwezi kuhalalisha kuwadhuru raia wa Israeli tarehe 7 Oktoba. Na kile ambacho Hamas ilifanya tarehe 7 Oktoba hakiwezi kuhalalisha kuwadhuru raia wa Palestina tangu wakati huo."