Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa ni jambo la kusisimua nitaenda kuwasimulia wanafunzi – Maria Rulands

Maria Rulands, mwalimu kutoka Ujerumani anayefundisha katika shule ya mradi wa UNESCO nchini Ujerumani katika ziara na wanafunzi New York Marekani.
UN News/Anold Kayanda
Maria Rulands, mwalimu kutoka Ujerumani anayefundisha katika shule ya mradi wa UNESCO nchini Ujerumani katika ziara na wanafunzi New York Marekani.

Kutembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa ni jambo la kusisimua nitaenda kuwasimulia wanafunzi – Maria Rulands

Na Anold Kayanda
Utamaduni na Elimu

Maria Rulands, mwalimu kutoka Ujerumani, anaielezea ziara yake ya hivi ya mwezi Agosti 2025 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani kuwa uzoefu wa maana sana, akisema imekuwa “ya maana” na “ya kweli” kwa kazi yake ya ualimu.

Rulands, anayefundisha katika shule ya mradi wa UNESCO nchini Ujerumani, anasema ziara hiyo imempa fursa ya kipekee kushuhudia diplomasia ya kimataifa ikitekelezwa kwa vitendo. “Shule yetu inajihusisha sana katika kukuza demokrasia, uhuru, na elimu ya amani,” anaeleza akifafanua zaidi kwamba kuwa hapa katika Umoja wa Mataifa ni “jambo la kusisimua kunafanya kila tunachofundisha kuwa halisi.”

Mwalimu Maria Rulands anasisitiza thamani ya kushuhudia mazingira ya Umoja wa Mataifa kwa macho yake mwenyewe, akisema kuwa uzoefu huo utaimarisha mafundisho yake kuhusu ushirikiano wa kimataifa na ujenzi wa amani. Anasema, “nitakaporejea Ujerumani, nitaweza kuzungumza na wanafunzi wangu si kutoka vitabuni tu, bali pia kutokana na uzoefu wangu binafsi.”.

Miongoni mwa mambo yaliyoleta furaha katika ziara yake ni nafasi ya kuketi kwenye moja ya viti vya maonesho yaliyowekwa kukumbushia historia ya mkutano uliofanyika mjini San Fransisco kulikozaliwa Umoja wa Mataifa na kutiwa saini kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Juni 26, 1945. “Umekuwa wakati wa kujivunia,” anasema Rulands. “Kusaini ahadi kwa maadili ya Umoja wa Mataifa, kwa demokrasia na amani nimehisi kuheshimiwa sana.”

Ziara yake imekuja wakati ambapo juhudi za kimataifa katika elimu zinaweka msisitizo zaidi kwenye ujifunzaji wa uzoefu wa moja kwa moja na uwajibikaji wa kijamii. Kwa Rulands, Umoja wa Mataifa si tu alama ni darasa linaloishi.