WHO na UNICEF watoa wito kwa serikali kuwekeza katika mifumo ya kusaidia unyonyeshaji
WHO na UNICEF watoa wito kwa serikali kuwekeza katika mifumo ya kusaidia unyonyeshaji
Wakati dunia ikiadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani (Tarehe 1-7 Agosti), wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya duniani WHO na lile la masuala ya Watoto UNICEF wametoa tamko la pamoja wakisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mifumo thabiti ya kusaidia unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa hii leo kutoka Geneva Uswisi na New York Marekani wakuu hao wamesema unyonyeshaji ni njia bora ya kuhakikisha afya, ukuaji na uhai wa mtoto katika hatua za mwanzo za maisha, ukiwa kama chanjo ya kwanza dhidi ya magonjwa kama kuhara na nimonia.
Pamoja na faida kubwa za unyonyeshaji maziwa ya mama bado kuna changamoto kwani ni asilimia 48 pekee ya watoto chini ya miezi sita wanaonyonyeshwa ipasavyo. Hili ni chini ya lengo la asilimia 60 ifikapo 2030 na hii imesema inasababishwa na changamoto mtambuka zinazohusisha wakina mama wenye watoto wachanga, wahudumu wa afya na mifumo ya afya.
Mapendekezo
Chini ya kauli mbiu ya mwaka huu ya “Wekeza kwenye unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama, Wekeza kwenye mustakabali” WHO na UNICEF wametoa wito kwa serikali, wasimamizi wa afya na wadau wengine kuwekeza katika usaidizi wa hali ya juu wa kunyonyesha, na kutoa mapendekezo sita ambayo ni:
- Uwekezaji katika huduma bora na za usawa kwa mama na watoto wachanga, zikiwemo huduma za kusaidia unyonyeshaji;
- Kuongeza bajeti za kitaifa kwa ajili ya programu za unyonyeshaji;
- Kuweka kipengele cha ushauri na msaada wa unyonyeshaji kwenye huduma za afya ya mama na mtoto;
- Kuwajengea uwezo wahudumu wa afya kuhusu unyonyeshaji, hata katika mazingira ya dharura;
- Kuimarisha mfumo wa afya ya jamii ili kusaidia mama hadi mtoto atimize miaka miwili au zaidi;
- Kulinda unyonyeshaji kwa kufuata Kanuni ya Kimataifa ya uuzaji wa vifaa mbadala vya maziwa ya mama.
WHO na UNICEF wamesisitiza kuwa kuimarisha mifumo ya afya kwa ajili ya unyonyeshaji si tu hitaji la kiafya, bali pia ni suala la maadili na uchumi.